****
Katika hatua inayotarajiwa kuleta mabadiliko katika upatikanaji wa huduma nchini, kampuni ya Sihebs Technologies Co. Ltd imezindua rasmi jukwaa la kidijitali la Mr Raha, linalolenga kuunganisha wateja na watoa huduma waliothibitishwa kwa njia rahisi, salama na yenye ufanisi.
Uzinduzi huo umefanyika Jumatano, Juni 24, 2026, katika ukumbi wa PSSSF Victoria House jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya teknolojia, biashara na vyombo vya habari.
Jukwaa la Mr Raha linapatikana kupitia tovuti yake pamoja na programu ya simu inayoweza kupakuliwa kupitia Google Play. Mfumo huo umeundwa kuwasaidia wananchi kupata huduma wanazohitaji kwa urahisi huku ukiwawezesha watoa huduma kufikia wateja wengi zaidi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Mr Raha, Siwangu Mgata, alisema jukwaa hilo limebuniwa kujenga mazingira ya uaminifu kati ya wateja na watoa huduma.
Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Mr Raha, Siwangu Mgata akizungumza na Waandishi wa habari Mapema Leo.Alieleza kuwa mfumo huo unatumia mbinu za kidijitali kuhakikisha huduma zinapatikana kutoka kwa watu waliothibitishwa, jambo linaloongeza usalama na kuondoa changamoto ya kupata watoa huduma wasioaminika.
Kwa upande wa watoa huduma, Mr Raha inatoa fursa ya kujitangaza na kuwafikia wateja wapya kwa gharama nafuu. Wakati huo huo, wateja wanapata uhakika wa kupata huduma kutoka kwa wataalamu waliokaguliwa na kuthibitishwa.
Kampuni hiyo pia imeanzisha mtandao wa washirika wa usajili ambao watakuwa na jukumu la kuthibitisha na kuorodhesha watoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Uzinduzi wa Mr Raha unaenda sambamba na ukuaji wa jumuiya ya TeamRaha, ambayo inatarajiwa kukutana katika tamasha la TeamRaha Beach Party litakalofanyika Juni 27, 2026 katika Ununio Beach Park.
Sihebs Technologies Co. Ltd ni kampuni ya Kitanzania inayojihusisha na utoaji wa suluhisho za TEHAMA kwa biashara na jamii, huku Mr Raha ikitajwa kuwa miongoni mwa miradi yake mikubwa inayolenga kubadilisha sekta ya huduma kupitia teknolojia.










Post a Comment