******
Chuo Kikuu cha Mzumbe kimesema kitafanya tafiti za kina kubaini maeneo yenye fursa za uwekezaji kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), hatua inayolenga kuisaidia Serikali kufanya maamuzi ya uwekezaji yanayozingatia ushahidi wa kisayansi.
Hatua hiyo pia inalenga kuimarisha mchango wa chuo katika maendeleo ya taifa kupitia tafiti, mafunzo na ushauri wa kitaalamu kuhusu utekelezaji wa miradi ya ubia.
Akizungumza wakati wa mhadhara ya kujenga uwezo kuhusu PPP yaliyofanyika chuoni hapo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Profesa Hawa Tundui amesema Mzumbe imechagua PPP kuwa moja ya maeneo ya kimkakati ya utafiti kutokana na mchango wake katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
"Tunataka kufanya tafiti zitakazotusaidia kubaini fursa zilizopo katika eneo la PPP na kuishauri Serikali kuhusu maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele. Hili ni eneo jipya lenye fursa nyingi, hivyo kama wanataaluma tuna wajibu wa kulifanyia kazi," amesema.
Amesema jukumu la chuo kikuu haliishii kufundisha wanafunzi pekee, bali pia kuzalisha maarifa na ushahidi wa kitaalamu unaoweza kusaidia kutatua changamoto za maendeleo nchini.
"Leo si wanafunzi pekee wanaojifunza, hata sisi wanataaluma tupo hapa kujifunza. Maarifa tunayoyapata yatatusaidia kuyafikisha kwa jamii na kuyatumia kutoa ushauri wa kitaalamu," amesema.
Amesema mhadhara huo, uliofanyika kwa ushirikiano na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), umeongeza idadi ya wataalamu wa chuo wenye uwezo wa kufundisha masuala ya PPP na kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma, sekta binafsi na wadau wengine.
"Sasa tuna wataalamu wenye uwezo wa kushirikiana na PPP Centre kuandaa na kutoa mafunzo mafupi ya kitaaluma kwa watumishi wa umma, sekta binafsi na wadau wengine wanaohitaji kuongeza uelewa kuhusu PPP," amesema.
Ameongeza kuwa chuo kitaendelea kuandaa programu za mafunzo mafupi pamoja na kuhamasisha tafiti zitakazobaini maeneo ambayo hayajafanyiwa utafiti wa kutosha ili kutoa ushahidi utakaosaidia Serikali katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala Profesa Allen Mushi amsema Mzumbe pia inakusudia kutumia mfumo wa PPP kuboresha miundombinu ya chuo na kuanzisha programu mpya za taaluma zinazokidhi mahitaji ya soko.
Amesema tayari chuo kimeanza mazungumzo na PPP Centre kuhusu namna ya kutumia mfumo huo kugharamia baadhi ya miradi ya maendeleo ya chuo, huku kikitarajia kupanua ushirikiano katika maeneo ya utafiti na kujenga uwezo wa wahadhiri.
"Tanzania sasa inaungana na mwelekeo wa dunia wa kuhamasisha uwekezaji kutoka sekta binafsi. Kama taasisi ya elimu ya juu tuna wajibu wa kuhakikisha tunachangia maendeleo hayo kupitia tafiti, mafunzo na ubunifu," amesema.
Profesa huyo amesema Mzumbe pia inaangalia uwezekano wa kuanzisha kozi mpya, zikiwemo za shahada za uzamili katika masuala ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, ili kuzalisha wataalamu watakaosaidia kuimarisha utekelezaji wa miradi ya PPP nchini.
Amesema ushirikiano kati ya Mzumbe na PPP Centre utasaidia kuongeza tafiti katika eneo hilo, ambalo bado halijafanyiwa utafiti wa kutosha nchini, na kutoa maarifa yatakayosaidia Serikali, sekta binafsi na wadau wengine kufanya maamuzi yenye tija.
"Tunashukuru PPP Centre kwa kutuchagua. Tunalichukulia jambo hili kuwa mwanzo wa ushirikiano wenye manufaa makubwa kwa chuo chetu na kwa maendeleo ya nchi," amesema.
Mwisho











Post a Comment