Vijana 130 wa dini ya Kiislamu leo Juni 7, 2026 wamefungishwa ndoa za pamoja katika hafla iliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikma Foundation wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo imewakutanisha maharusi kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo kuwasaidia vijana wanaokabiliwa na changamoto za gharama za ndoa kuanzisha familia kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Ndoa hizo zimesimamiwa na Mkurugenzi wa Al-Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki, ambaye amekuwa akiendesha mpango huo kwa miaka kadhaa.
Mkurugenzi wa Al-Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki.Hafla hiyo pia imeongozwa na Rais wa taasisi hiyo, Sheikh Shareef Abdulgadir.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobass Katambi, ambaye ameipongeza Al-Hikma Foundation kwa kuwezesha vijana hao kufunga ndoa halali.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobass Katambi.Katambi alisema taasisi hiyo imeonyesha mfano mzuri kwa kuandaa mchakato wa awali uliowahusisha washiriki katika mahojiano, uchunguzi wa kina pamoja na kugharamia mahari kwa maharusi wa kiume.
Alisema mmomonyoko wa maadili katika jamii unachangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la mahusiano yasiyo halali na migogoro ya kifamilia, hivyo ndoa za pamoja ni sehemu ya suluhisho la changamoto hizo.
“Ndoa halali hujenga familia halali, na familia ndiyo msingi wa jamii imara na taifa lenye maendeleo,” alisema Katambi.
Kwa upande wake, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad, amewataka wanandoa wapya kujenga utamaduni wa kuvumiliana na kutatua migogoro kwa mazungumzo badala ya kutishiana kuachana.
Alisema tabia ya kutumia kauli za kuachana kila panapotokea hitilafu ndogo ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuvunjika kwa ndoa na familia nyingi.
Sheikh Walid alisema ndoa ni taasisi inayohitaji uvumilivu, maelewano na hekima katika kutatua tofauti zinazojitokeza katika maisha ya kila siku.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini pamoja na wananchi waliokusanyika kushuhudia tukio hilo kubwa la kijamii na kidini jijini Dar es Salaam.













Post a Comment