PROF. SHEMDOE AELEKEZA MAAFISA UTUMISHI WALIOKWAMISHA WATUMISHI KUPANDA MADARAJA KUCHUKULIWA HATUA

******

Na OWM - TAMISEMI, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemuelekeza Katibu Mkuu - UTUMISHI Bw. Juma Selemani Mkomi kufanya tathmini ya kubaini Maafisa Utumishi waliozembea kukamilisha mchakato wa Watumishi wa Umma kupandishwa madaraja kwa mwaka wa fedha 2025/26 na kuwachukulia hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria, Taratibu, Kanuni na Miongozo ya Utumishi wa Umma. 

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo Juni 23, 2026 kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

“Kuna Maafisa Utumishi kwa uzembe wamesababisha watumishi kutopandishwa madaraja mwaka 2025/26, Katibu Mkuu UTUMISHI kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi nakuelekeza kufanya tathmini ya kubaini maafisa waliokwamisha upandishaji wa madaraja na kuchukua hatua ya kuwaondoa katika nafasi zao,” amesisitiza Prof. Shemdoe. 

Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Taasisi za Umma na Maafisa Utumishi nchini kushughulikia kwa wakati kero na malalamiko ya watumishi wanaowaongoza, kwani nafasi walizonazo ni kwa ajili ya kuwatumikia watumishi hao ili nao waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Pia, Prof. Shemdoe amemuelekeza Katibu Mkuu UTUMISHI kumpatia ajira ya kudumu kijana mlemavu aliyemkuta kwenye banda la VETA ambaye hana mikono lakini ana ujuzi wa kusanifu majengo na samani kwa kutumia miguu yake kupitia kompyuta mpakato.

Aidha, Prof. Shemdoe kwa niaba ya watumishi wa umma nchini amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapandisha madaraja watumishi wa umma, kulipa madai ya muda mrefu ya watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi wengi wa kada mbalimbali wakiwemo walimu na wa sekta ya afya.  

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amezipongeza taasisi za kifedha zikiwemo CRDB, NMB, AZANIA, NBC na nyinginezo zilizoshiriki maonesho ya Wiki ya Wiki ya Utumishi wa Umma kutokana na kuhitajika kwa taasisi hizo kwa watumishi wa umma, ambako kunawapa wigo watumishi kuchagua benki wanayoona inafaa kuchukua mkopo wa kuwezesha shughuli zao binafsi za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Selemani Mkomi amesema kupitia maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu, wananchi wamepata huduma za moja kwa moja kutoka katika taasisi za umma na kuongeza kuwa, taasisi za umma zimepata fursa ya kubadilishana uzoefu kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Serikali kupata mrejesho utakaoiwezesha kuborsha utoaji wa huduma.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, jumla ya Taasisi za Umma 226 zimetoa elimu na huduma mbalimbali kwa watumishi wa umma na wananchi ikiwemo matumizi ya mifumo ya utoaji wa huduma katika Utumishi wa Umma, hati za viwanja, vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya taifa na huduma za kitabibu za kibingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Benjamini Mkapa, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa (MOI) na Hospitali ya Bugando.












 

0/Post a Comment/Comments