Dar es Salaam
Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa mafanikio ya mfumo wa fedha hayana budi kwenda sambamba na ustawi wa mwananchi mmoja mmoja pamoja na ukuaji wa sekta binafsi nchini.
Amesema kuwa kipimo cha mafanikio kisiishie kwenye idadi ya wananchi waliofikiwa na huduma za fedha, bali kijikite katika namna huduma hizo zinavyokuza mitaji, biashara ndogo ndogo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mhe. Samia ameyasema hayo Juni 12, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria Maadhimisho ya Miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Aidha, Rais Samia amesema serikali itaendelea kuimarisha mazingira wezeshi ya sekta ya fedha ili kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wengi zaidi kwa ufanisi na usawa.
Katika maadhimisho hayo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa Benki Kuu imeendelea kuhakikisha huduma za mifumo ya malipo nchini zinakuwa bora, salama na za uhakika.
Amesema maboresho ya mifumo ya malipo yameendelea kufanyika kupitia mifumo ya Interbank Settlement System (TISS), Tanzania Automated Clearing House (TACH/TOUCH), pamoja na mifumo ya kukusanya na kusafisha hundi.
Aidha, amesema mifumo ya miamala midogo kama Electronic Fund Transfer (EFT) na Tanzania Instant Payment System (TIPS) imeendelea kuimarishwa sambamba na ukuaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi na maendeleo ya TEHAMA.
“Kwa sasa benki zote nchini zinatoa huduma zake kidijitali, jambo ambalo limeongeza ufanisi wa mifumo ya malipo na kurahisisha huduma kwa wananchi,” amesema Tutuba.
Ameongeza kuwa malipo makubwa ya serikali pamoja na ukusanyaji wa mapato ya kodi yanaendelea kufanyika kupitia mifumo ya kielektroniki inayosimamiwa na Benki Kuu, hatua iliyosaidia kuongeza ufanisi na kupunguza gharama.
Kwa upande wa akiba ya fedha za kigeni, Gavana Tutuba amesema sekta ya nje imeendelea kuwa himilivu na thabiti ambapo kwa zaidi ya miaka 25 Benki Kuu imeendelea kujenga na kulinda akiba hiyo.
Amesema akiba ya fedha za kigeni kwa sasa inatosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi 4.8, kiwango ambacho kiko juu ya kiwango cha kisheria cha miezi minne.
Aidha, amesema Benki Kuu imeendelea kuimarisha akiba hiyo kupitia mpango wa ununuzi wa dhahabu ulioanza Oktoba 2024, ambapo BoT inanunua dhahabu kwa kutumia shilingi ya Tanzania ili kuongeza akiba ya fedha za kigeni.
Amebainisha kuwa mpango huo umefanikisha kuongeza mgawanyo wa akiba na kuhakikisha rasilimali za taifa zinachangia moja kwa moja katika utulivu wa fedha nchini huku ukiwanufaisha wadau wa sekta ya madini.
“Mpaka Juni 10, 2026 Benki Kuu ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa tani 27.05 zenye thamani ya takribani shilingi trilioni 10,” amesema Tutuba.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na mageuzi yaliyofanywa na serikali, ushirikiano na sekta ya madini, pamoja na usimamizi madhubuti wa kisheria ulioongeza uwazi na ufanisi katika sekta hiyo.






Post a Comment