RC SENYAMULE AKAGUA MIRADI DABALO, AWATAKA WAKULIMA KUKUMBATIA STAKABADHI GHALANI

.....

Na Carlos Claudio, Chamwino

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu, maji na kilimo.

Senyamule aliyasema hayo Juni 15, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Kata ya Dabalo, Wilaya ya Chamwino, ambapo alitembelea mradi wa maabara katika Shule ya Sekondari Dabalo na mradi wa maji unaotekelezwa katika Kitongoji cha Muungano.

Akizungumza baada ya kukagua maabara hiyo, Senyamule alisema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya mradi huo kwani jengo limekamilika na tayari wanafunzi wanatumia maabara hiyo kwa mafunzo ya vitendo katika masomo ya sayansi.

Alisema uwepo wa maabara utawajengea wanafunzi hamasa ya kujifunza masomo ya sayansi na kuongeza uelewa wao kutokana na kupata nafasi ya kufanya majaribio kwa vitendo.

“Watoto wetu wakiongezeka katika masomo ya sayansi tunapata wataalamu wengi zaidi, wakiwemo madaktari, wahandisi na wabunifu mbalimbali watakaosaidia maendeleo ya taifa. Haya ni matokeo ya dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza katika elimu na kuongeza wataalamu nchini,” alisema Senyamule.

Katika mradi wa maji wa Kitongoji cha Muungano unaofadhiliwa na Shirika la World Vision, Mkuu huyo wa Mkoa alisema mradi huo umeongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Dabalo na maeneo jirani.

Aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira yanayowezesha taasisi za maendeleo kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi.

Senyamule alisema lengo la Serikali kukagua miradi ya maendeleo ni kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatumika ipasavyo na kwamba wananchi wanapata huduma zinazokusudiwa bila kujali kama miradi hiyo inatekelezwa na Serikali au sekta binafsi.

Wakati akizungumza na wananchi na kutatua kero mbalimbali za kijiji hicho, Senyamule aliwataka wakulima kuendelea kuamini na kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani, akisema umeondoa changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili hapo awali.

Alisema historia inaonesha kuwa kabla ya mfumo huo kuwepo, baadhi ya wakulima walikuwa wakipunjwa kupitia mizani isiyo sahihi pamoja na kukosa masoko ya uhakika ya mazao yao.

“Serikali iliona ni muhimu kuweka mfumo utakaowawezesha wakulima kupata bei sahihi, vipimo sahihi na masoko ya uhakika. Aidha, mfumo huu unasaidia kuhakikisha mazao yanayouzwa nje yanakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa katika masoko ya kimataifa,” alisema.

Aliongeza kuwa mafanikio ya mauzo ya mazao kama ufuta, mbaazi na mazao mengine yanatokana na jitihada za Serikali kuweka mazingira mazuri ya biashara, mahusiano ya kimataifa na mikataba inayowezesha upatikanaji wa masoko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja, alisema mfumo wa stakabadhi ghalani unaendelea kuimarika katika eneo la Dabalo ambapo wakulima wameanza kuona manufaa yake kupitia bei nzuri zinazopatikana katika minada.

Alisema awali kulikuwa na changamoto kutokana na uwepo wa wafanyabiashara waliokuwa wakinunua mazao moja kwa moja vijijini, lakini baada ya wakulima kushuhudia bei zinazopatikana kupitia mnada, wengi wameanza kupeleka mazao yao kwenye ghala rasmi.

“Mwaka jana kulikuwa na changamoto za uongozi katika chama cha ushirika, lakini baada ya kufanyika mabadiliko, mfumo umeendelea vizuri. Wananchi sasa wanajionea wenyewe faida za kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na elimu ya vitendo inaendelea kutolewa,” alisema Mayanja.

Alibainisha kuwa mwitikio wa wakulima kupeleka ufuta kwenye ghala umeongezeka kutokana na kuridhishwa na bei zinazopatikana kupitia mfumo huo, jambo linaloendelea kuimarisha mapato yao na ustawi wa jamii kwa ujumla.



 

0/Post a Comment/Comments