Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi imezitaka taasisi zote zilizoanza mchakato wa usajili lakini hazijaukamilisha, kuhakikisha zinakamilisha usajili huo ndani ya siku saba za kazi kuanzia leo.
Aidha, taasisi ambazo bado hazijaanza kabisa mchakato wa usajili zimetakiwa kuanza na kuukamilisha ndani ya kipindi hicho cha siku saba.
Tume hiyo pia imezitaka taasisi zote kujiandaa kwa ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ambao tayari umeanza na utaendelea kufanyika kwa kipindi chote.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 12, 2026, Mkurugenzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Dkt. Emmanuel Mkilia, alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha taasisi zote zinazingatia matakwa ya sheria na kulinda taarifa za wananchi.
Dkt. Mkilia alisema wananchi pia wanapaswa kulinda taarifa zao binafsi kwa mujibu wa sheria na kutoa taarifa au malalamiko kwa tume endapo watabaini matumizi yasiyo halali ya taarifa zao au ukiukwaji wa faragha zao.
Aliongeza kuwa tume itaendelea kutoa elimu, miongozo na usimamizi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo imara wa ulinzi wa taarifa binafsi unaolinda haki za wananchi na kuimarisha imani katika matumizi ya teknolojia na huduma za kidijitali.


Post a Comment