TAKUKURU TEMEKE YAWAOKOLEA MADEREVA BAJAJI SHILINGI 370,000 KIGAMBONI

****

 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikiwa kurejesha Sh. 370,000 kwa madereva bajaji 40 wa Kituo cha Kibada kilichopo Halmashauri ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Mafanikio hayo yameelezwa leo Juni 2, 2026 na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Francis Luena, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo.

Luena amesema madereva hao walitozwa fedha hizo kwa njia isiyo halali wakidaiwa kulipia stika za maegesho, jambo lililosababisha malalamiko na kuibua uchunguzi.

Amesema uchunguzi uliofanywa kwa ushirikiano kati ya TAKUKURU, viongozi wa madereva na vyombo vya dola ulithibitisha kuwepo kwa udanganyifu huo.

“Fedha zimerejeshwa kwa wahusika na hatua stahiki zimechukuliwa. Aidha, hali ya utulivu na amani katika kituo hicho imeendelea kuimarika,” amesema Luena.

Katika hatua nyingine, amesema TAKUKURU Mkoa wa Temeke imepokea malalamiko 68 katika robo ya Januari hadi Machi mwaka huu.

Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 41.7 ikilinganishwa na robo iliyotangulia, hali ambayo amesema inaonyesha kuongezeka kwa imani ya wananchi kwa taasisi hiyo pamoja na utayari wao wa kuripoti vitendo vya rushwa.

Kwa mujibu wa Luena, asilimia 76.5 ya malalamiko yaliyopokelewa yanahusu tuhuma za rushwa na yanaendelea kufanyiwa uchunguzi kwa ajili ya kuthibitisha ukweli wake na kuchukua hatua za kisheria pale itakapobainika.

Amesema malalamiko yasiyohusu rushwa yamepungua kutoka asilimia 54.2 katika robo iliyopita hadi asilimia 23.5 katika kipindi cha sasa.

Malalamiko hayo yameshughulikiwa kwa kutoa elimu kwa wananchi, huku baadhi yakipelekwa kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.

Kuhusu mashtaka, Luena amesema kesi moja mpya imefunguliwa mahakamani katika kipindi hicho, na kufanya jumla ya kesi tano za rushwa kuendelea kusikilizwa.

Amesema TAKUKURU Mkoa wa Temeke utaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali katika robo ya Aprili hadi Juni 2026, ikiwemo kufuatilia utekelezaji wa maazimio na mapendekezo yaliyotolewa kwenye vikao vya mashauriano kati ya taasisi hiyo na wadau wake.







0/Post a Comment/Comments