Na Carlos Claudio, Dodoma.
Chama cha Wauguzi Tanzania (TANA) kimelaani vikali vitendo vya unyanyasaji, ukatili na udhalilishaji dhidi ya watumishi wa afya katika maeneo yao ya kazi, kikisisitiza kuwa matukio hayo yanahatarisha usalama wa watumishi, wagonjwa na ubora wa huduma za afya nchini.
Akizungumza jijini Dodoma, Rais wa TANA, Dkt. Ezekiel Mbao, alisema chama hicho kimepokea kwa masikitiko taarifa za muuguzi aliyedaiwa kushambuliwa na daktari akiwa kazini katika Hospitali ya Mji wa Bariadi, mkoani Simiyu, Mei 26, 2026.
Dkt. Mbao alisema TANA ilipokea taarifa za tukio hilo Mei 27, 2026 na kuanza kufuatilia kwa karibu mwenendo wake kwa kushirikiana na viongozi wa chama mkoani Simiyu pamoja na mamlaka husika.
Alisema tukio hilo si mgogoro wa kawaida kati ya watu wawili bali ni suala linalogusa heshima, utu na usalama wa watumishi wa afya pamoja na hadhi ya taaluma ya uuguzi.
“Tunalaani na kukemea vikali vitendo vyote vya unyanyasaji, ukatili na uzalilishaji dhidi ya watumishi wa afya katika maeneo yao ya kazi. Kulinda heshima na usalama wa muuguzi ni kulinda ubora wa huduma za afya kwa Watanzania,” alisema Dkt. Mbao.
Kwa mujibu wa TANA, kitendo hicho kilimdhalilisha muuguzi akiwa katika mazingira yake ya kazi, kikahatarisha usalama wake pamoja na wa mgonjwa aliyekuwa akihudumiwa na wagonjwa wengine waliokuwa karibu na eneo la tukio.
Dkt. Mbao alisema matukio ya aina hiyo huathiri mshikamano wa watumishi wa afya na kusababisha kushuka kwa ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa kumpiga au kumshambulia mtumishi mwenzako kazini ni kosa la jinai, kitaaluma na kiutumishi, hivyo wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa bila kujali taaluma, cheo au nafasi zao.
Aidha, TANA imezitaka mamlaka zote zenye dhamana ya kusimamia taaluma, sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi kutekeleza majukumu yao kwa haki, usawa na bila upendeleo ili kuhakikisha mazingira salama ya kazi kwa watumishi wa afya.
“Tukio la namna hii linahitaji kushughulikiwa kwa wakati na kwa uwazi ili kuondoa taharuki miongoni mwa watumishi na kulinda mazingira bora ya kazi,” alisema.
Dkt. Mbao alisema chama hicho kitaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya suala hilo kupitia viongozi wa tawi la Simiyu na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha usalama wa mazingira ya kazi kwa wauguzi na watumishi wengine wa afya nchini.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wauguzi Tawi la Hospitali ya Benjamin Mkapa, Mwagu Thobias, amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa za matukio yanayotokea maeneo ya kazi badala ya kuyaficha.
Alisema kuchelewa kwa taarifa za tukio hilo kutoka kwa mamlaka husika kulisababisha suala hilo kujulikana zaidi kupitia vyombo vya habari, jambo ambalo halipaswi kujirudia.
Mwagu alizitaka mamlaka kuhakikisha sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa inazingatiwa ili kulinda usalama na uhai wa wauguzi ambao ni sehemu kubwa ya nguvu kazi katika utoaji wa huduma za afya.



Post a Comment