*****
Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa inaendelea kunufaika na ushirikiano wa kiuchumi na China unaofungua fursa mpya za biashara na uwekezaji kwa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Mapema Leo, Balozi wa Tanzania nchini China, Dkt. Suleiman Haji Suleiman, amesema bidhaa za Tanzania zinaweza kuingia katika soko la China bila ushuru endapo zitakidhi vigezo vinavyotakiwa.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika moja ya masoko makubwa duniani na kuinua pato la taifa.
Kwa mujibu wa balozi huyo, biashara kati ya Tanzania na China ilifikia thamani ya Dola za Marekani bilioni 23.2 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025.
Hata hivyo, amedai Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.8 pekee, huku bidhaa nyingi zaidi zikiagizwa kutoka China.
Amebainisha kuwa changamoto kubwa ni uzalishaji mdogo na utegemezi wa kuuza bidhaa ghafi bila kuziongezea thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
Balozi huyo alisema ubalozi unaendelea kuvutia wawekezaji wa China kuwekeza katika sekta za viwanda, teknolojia na mitambo ya kisasa ya uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Ubalozi wa Tanzania nchini China umetangaza kuanzisha kliniki maalumu ya biashara katika Maonesho ya Sabasaba kwa ajili ya kutoa ushauri kwa wafanyabiashara.
Amesema huduma hiyo itawawezesha Watanzania kupata elimu kuhusu fursa za soko la China, taratibu za biashara, uwekezaji na upatikanaji wa mitambo ya viwandani.





Post a Comment