Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mahimbali amesema TEMESA imejipanga kuhakikisha huduma za ufundi na matengenezo ya magari ya Serikali zinatolewa kwa viwango vya juu kwa kutumia teknolojia za kisasa na za viwango vya kimataifa.
“TEMESA inaona fursa kubwa katika kuimarisha ushirikiano na TOYOTA kupitia miradi ya pamoja itakayowezesha taasisi hizi mbili kubadilishana utaalamu kwa mafundi na kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wadau wetu,” amesema Mtendaji Mkuu.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa TOYOTA Tanzania, Bw. Jatin Pandya amehakikisha utayari wa kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na TEMESA katika mafunzo ya kitaalamu kwa mafundi, ushauri wa kiufundi, matumizi ya teknolojia mpya na kuimarisha mifumo ya usalama wa magari.
“Sisi TOYOTA tunatanguliza usalama wa watumiaji wa magari na ubora wa huduma. Tunaamini ushirikiano huu utachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za matengenezo ya magari nchini na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani,” amesisitiza Pandya.
Aidha, mara baada ya kikao hicho, Mtendajji mkuu pia alipata fursa ya kufanya ziara fupi katika karakana za TOYOTA ili kujionea teknolojia mpya zinazotumika katika matengenezo ya magari.
Miongoni mwa mambo waliyojadili katika kikao hicho ni pamoja na uwezekano wa kuanzisha ushirikiano kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi - PPP. Hatua inayotarajiwa kuimarisha uwezo wa karakana na kuongeza ufanisi wa huduma katika sekta ya matengenezo ya magari.
Kikao hicho kimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya TEMESA na TOYOTA, huku kikitarajiwa kuwa chachu ya mageuzi makubwa katika sekta ya ufundi wa magari nchini.







Post a Comment