TOSCI YAWATAKA WAFANYABIASHARA KUUZA MBEGU ZILIZO SAJILIWA

.......

NA Ester Maile Dodoma 

Mtafiti na Mkaguzi wa Mbegu kutoka Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Neema Yohana, amesema taasisi hiyo inaendelea kutumia Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika Chinangali, jijini Dodoma, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya mbegu bora pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wakulima katika sekta ya mbegu.

Akizungumza na waandishi wa habari Neema amesema TOSCI pia imebaini kuwa wafanyabiashara wengi wa mbegu hawana mafunzo ya kutosha kuhusu biashara hiyo, hivyo taasisi imekuwa ikiwapatia elimu na mafunzo ili kuhakikisha wanazingatia viwango vinavyotakiwa katika usambazaji wa mbegu bora.

Aidha, amesema TOSCI inaendelea kuelimisha wananchi namna ya kutambua mbegu halisi na kutofautisha na mbegu bandia kwa kuangalia lebo zilizowekwa kwenye vifungashio vya mbegu.

Amewahimiza wakulima kununua mbegu kutoka kwa wauzaji waliosajiliwa na TOSCI, pamoja na kukwangua lebo ya uhakiki na kufuata maelekezo yaliyopo kwenye kifungashio. 

Amesema mbegu ikiwa imethibitishwa na kusajiliwa, mnunuzi atapokea ujumbe mfupi kupitia simu yake ya mkononi unaothibitisha kuwa mbegu hiyo ni halisi na imekidhi viwango vya ubora.



 

0/Post a Comment/Comments