*****
Umoja wa Maimamu na Walimu wa Madrasa Tanzania (UMATA) umetoa wito kwa viongozi wa dini, serikali na wananchi kwa ujumla kuendelea kuzingatia misingi ya amani ili kulinda utulivu uliopo nchini.
Akizungumza kuhusu hali ya kijamii na kisiasa, Mwenyekiti wa Kitaifa wa UMATA, Sheikh Arif Surya, alisema ni muhimu kwa Watanzania kuendeleza mshikamano na kuepuka vitendo vinavyoweza kuzua taharuki au migawanyiko katika jamii.
Alisema taifa limeendelea kunufaika na mazingira ya amani kwa muda mrefu, hivyo kuna ulazima wa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha hali hiyo inadumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Sheikh Surya alieleza kuwa matukio ya mikusanyiko isiyo na utaratibu yanaweza kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii, pamoja na kusababisha madhara kwa wananchi wanaotegemea shughuli za kila siku kujipatia kipato.
Aidha, aliwataka wananchi kuwa waangalifu dhidi ya watu wanaoweza kutumia fursa za mikusanyiko hiyo kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa watu na mali zao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UMATA, Sheikh Abuu Ayman, aliwahimiza Watanzania kuendelea kushirikiana na vyombo husika katika kulinda utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa umoja, amani na maendeleo ni nguzo muhimu zinazopaswa kupewa kipaumbele na kila mwananchi.







Post a Comment