Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema usafiri kupitia Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) i
Umekuwa chaguo muhimu kwa wananchi wengi kutokana na usalama wake, uhakika wa ratiba na gharama nafuu za usafiri.
Akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Juni 22, 2026, Profesa Mbarawa amesema, huduma ya usafiri wa abiria kwa kutumia reli ya SGR ilianza mwezi Juni mwaka 2024 na hadi sasa zaidi ya abiria milioni sita wameshasafirishwa kupitia reli hiyo.
Amefafanua kuwa kwa sasa kila siku kuna treni nne zinazofanya safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa pande zote mbili, huku pia kukiwa na treni tatu zinazofanya safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro.
“Kwa wastani tunasafirisha takribani abiria 11,000 kila siku. Usafiri wa SGR umekuwa chaguo muhimu na kubwa kwa wananchi wote,” alisema Profesa Mbarawa.
Amebainisha kuwa wabunge, viongozi na wananchi kwa ujumla wameendelea kuuchagua usafiri huo kutokana na sababu tatu kuu ambazo ni usalama, uhakika wa ratiba pamoja na gharama nafuu.
“Katika usafiri wa SGR hakuna kuchelewa kwa ratiba. Vilevile nauli zake ni nzuri, nafuu na zinakubalika kwa wananchi wote,” alieleza
Mradi wa SGR ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati barani Afrika unaounganisha Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mbalimbali ya ndani ya nchi pamoja na nchi jirani.
Amesema mradi huo umeanzia Bandari ya Dar es Salaam kupitia Morogoro, Dodoma, Tabora, Shinyanga, Kigoma, huku ukiwa na lengo la baadaye kuunganisha Tanzania na nchi za Burundi pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa upande wa usafirishaji wa mizigo, Waziri huyo amesema huduma hiyo ilianza mwezi Juni mwaka 2025 na tayari mizigo imeanza kusafirishwa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuongeza ufanisi katika utoaji na usafirishaji wa mizigo kupitia reli hiyo ili kuongeza tija katika shughuli za biashara.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa kituo cha kuteremshia mizigo katika Malindi Wharf ndani ya Bandari ya Dar es Salaam, ambapo amesema mradi huo umefikia asilimia 99 ya utekelezaji.
Aidha, amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa kituo cha kisasa cha uhamishaji mizigo (Transhipment Centre) katika eneo la Bahi, kitakachowezesha mizigo kuhamishwa kutoka reli ya SGR kwenda reli ya MGR na kusafirishwa kuelekea Isaka, Mwanza pamoja na maeneo mengine nchini na hata Rwanda.
Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, miradi hiyo itapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo, kupunguza muda wa usafiri kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda maeneo mbalimbali ya Tanzania na nchi jirani pamoja na kuongeza manufaa ya kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Waziri huyo pia amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuharakisha utekelezaji wa mradi wa SGR, ambapo imeipatia Shirika la Reli Tanzania (TRC) takribani Shilingi trilioni 3.3 kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya reli vya Dodoma–Tabora na Tabora–Isaka.
Amesema fedha hizo zitasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili kufikia matarajio ya Serikali na wananchi ya kuwa na mtandao wa reli ya kisasa unaochochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.


Post a Comment