USHIRIKIANO WA DCEA NA VETA KUINUA MAISHA YA WALIOPONA URAIBU

******

Serikali imechukua hatua mpya ya kuwawezesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi yatakayowasaidia kujitegemea na kurejea katika maisha ya kawaida ya uzalishaji.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) jijini Dar es Salaam, Juni 4, 2026.

Makubaliano hayo yanalenga kuwapa ujuzi wa kazi waraibu waliomaliza matibabu ili waweze kujiajiri au kupata ajira, hatua inayotarajiwa kupunguza uwezekano wa kurejea katika matumizi ya dawa hizo.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha waliopona uraibu wanapata nafasi ya pili ya kujenga maisha yao.

Alisema waraibu waliopata nafuu wanahitaji zaidi ya matibabu pekee, kwani wanapaswa kuwezeshwa kiuchumi ili waweze kuwa sehemu ya nguvu kazi inayochangia maendeleo ya Taifa.

Lyimo alieleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya yanaendelea kuwa tishio kubwa katika jamii, hasa kwa vijana ambao ni nguzo muhimu ya maendeleo ya nchi.

Alibainisha kuwa athari za dawa hizo haziishii kwenye afya pekee, bali huathiri uchumi wa mtu binafsi, familia na Taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wake, matumizi ya dawa za kulevya pia huchochea ongezeko la vitendo vya uhalifu, migogoro ya kifamilia, kushuka kwa maadili pamoja na kupunguza nguvu kazi yenye tija.

Alisema Serikali kupitia DCEA imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulevya, kutoa elimu kwa umma na kuboresha huduma za tiba na urejeshaji.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa uzoefu umeonyesha kuwa matibabu pekee hayatoshi ikiwa waliopata nafuu hawatapatiwa fursa za kujiendeleza kiuchumi na kijamii.

"Wengi wanaopona uraibu hukumbana na changamoto za ajira, kipato na wakati mwingine hukataliwa na jamii. Hali hiyo inaweza kuwafanya kurejea tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Ndiyo maana ushirikiano huu na VETA una umuhimu mkubwa," alisema Lyimo.









0/Post a Comment/Comments