Baadhi ya wafanyabiashara wa Tarime waliopata mafunzo kupitia programu ya Local Business Development Program ya Barrick ambayo inazidi kufungua fursa kwa wafanyabiashara wazawa kunufaika na fursa za biashara kwenye migodi (picha kutoka Maktaba)

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko akiongea katika moja ya mafunzo yanayoendeshwa na kampuni kwa ajili ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara wazawa ili wachangamkie fursa za kibiashara zilizopo katika migodi ya Barrick (picha kutoka maktaba)
Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Kemanyaki inayotoa huduma mbalimbali katika mgodi wa Barrick North Mara wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wao Mkuu. Migodi ya Barrick imetoa fursa kwa wazawa kuanzisha makampuni ya kutoa huduma migodini na kutoa kipaumbele kutoa ajira kwa wananchi wanaotokea katika maeneo yanayozunguka migodi yake iliyopo Tarime na Msalala.
***
Wakati kampuni ya Barrick Mining Corporation imetoa ripoti ya utekelezaji wa masuala endelevu ya mwaka kipindi cha mwaka uliopita ikionyesha utendaji wa migodi yake sehemu mbalimbali duniani ambayo imebainisha suala la utekelezaji wa sera ya Maudhui ya Ndani (Local Content) kuendelea kupewa kipaumbele, migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu nchini inayoiendesha kwa ubia na serikali kupitia kampuni ya Twiga, inaendelea kutekeleza sera hii kwa ufanisi mkubwa na kunufaisha wafanyabiashara wengi na wananchi hususani wanaoishi maeneo yanayozunguka maeneo ya migodi hiyo.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa hadi mwaka jana asilimia 96% ya wafanyakazi wa Barrick sehemu mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania na asilimia 76% ya wazabuni wake walitoka katika nchi mwenyeji ambapo pia kampuni ilitumia zaidi ya dola bilioni $7.1 katika matumizi na wasambazaji wa ndani na nchi mwenyeji pia iliwekeza zaidi ya dola milioni 62 katika mipango ya maendeleo ya jamii.
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Hill akiongelea ripoti hiyo amesisitiza kuwa kampuni itaendelea kutekeleza sera zake madhubuti ambazo zinaendelea kuleta mafanikio.
"Tunapoingia katika awamu mpya ya kusisimua ya ukuaji na kupata mafanikio, uendelevu unasalia kuwa msingi wa jinsi tunavyofanya kazi. Kanuni ambazo zimetuongoza kwa miaka mingi bado hazijabadilika: kuwaweka watu wetu salama, uchimbaji madini kwa uwajibikaji, kujenga ushirikiano imara, na kutoa thamani ya muda mrefu ambayo inashirikiwa na washikadau wetu wote”,alisema.
Ushuhuda wa jinsi sera ya Maudhui ya ndani ina manufaa kwa watanzania wazawa wanaonufaika na fursa za zabuni za huduma mbalimbali za kibiashara katika migodi ya Barrick umetolewa na kampuni ya Kemanyanki Contractors, Manpower & General Supplies ambayo inatoa huduma mbalimbali katika mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara.
Akiongea juu ya mafanikio anayoendelea kuyapata kutokana na kampuni yake kufanya kazi na Barrick, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Nicolaus Mgaya alisema uwepo wa mgodi katika eneo lao kumefungua fursa za kiuchumi kwa wananchi kutokana na kupatiwa fursa ya biashara kupitia utekelezaji wa kanuni ya Maudhui ya ndani ambayo inazitaka kampuni za uchimbaji madini kuwajengea uwezo na kuwapa Watanzania fursa za biashara na ajira ili kukuza uchumi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ndogo ya The Mining (Local Content) Regulations ya Mwaka 2018.
Alisema mazingira kwa sasa katika migodi ya Barrick North Mara na Bulyanhulu ni mazuri na fursa ni nyingi, kinachohitajika kwa sasa ni wananchi wanaoishi jirani na migodi kuchangamkia fursa zilizopo na kuuona kama mali yao.
“Migodi hii kwa sasa ni wa kwetu na ni sehemu ya jamii - sio wa kuvamia”alisisitiza Mgaya.
Alisema kampuni ya Kemanyaki imekuwa ikipata zabuni mbalimbali za ujenzi na kutoa huduma katika mgodi wa Barrick North Mara ambapo kupitia zabuni hizo imeweza kutoa ajira zaidi ya 170 kwa kazi za kudumu na muda mfupi, wengi wao wakiwa vijana kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
Mgaya alisema wafanyakazi zaidi ya 600 wamenufaika na ajira katika kampuni yake katika kipindi cha kati ya mwaka 2023 na 2026, ambapo asilimia 90 ya ajira hizo ziligusa wakazi wa vijiji vilivyo jirani na mgodi.
“Asilimia 70 ya wafanyakazi wetu waliokuwa na hali duni - sasa hivi kupitia ajira hizi maisha yao yamebadilika kuwa bora ambapo wengi wao wamefanikiwa kujenga nyumba bora za kuishi na kuweza kusomesha watoto wao”,alisisitiza
Mkurugenzi Mgaya wakati akiongea katika hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, iliyofanyika hivi karibuni kwenye Hoteli ya CMG, mjini Tarime.
Mbali na ajira alisema kampuni ya Kemanyanki imekuwa ikisaidia jamii kwa kuchangia vifaa vya shule na michezo, kusaidia ada na michango ya shule kwa baadhi ya wafanyakazi wake na kufadhili walimu wa masomo ya sayansi katika shule zenye upungufu wa walimu hao
Alisema ajira zinazotolewa na kampuni yake ya Kemanyanki Group na makampuni mengine zimesaidia pia kupunguza wimbi la vijana ambao waliokuwa wakivamia mgodi wa Barrick North Mara kwa lengo la kuiba mawe ya dhahabu.
Takwimu kutoka serikalini zinaonesha kuwa kwa sasa vitendo vya uvamizi katika mgodi huo vimeshuka kwa asilimia 99, huku mahusiano ya mgodi na jamii yakiwa yameimarika zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Uwekezaji mkubwa kwenye mgodi wa North Mara umeshuhudia uwepo wa fursa nyingi za ajira kwa wazawa katika kampuni ya Barrick, lakini pia kwa wakandarasi wazawa wanaopata fursa za kibiashara mgodini hapo.
Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba hadi sasa mgodi wa Barrick North Mara umesajili kampuni zaidi ya 100, nyingi zikiwa za wazawa - ambazo zinapata fursa mbalimbali za kibiashara katika mgodi huo.
Barrick inaendeleza dhamira yake ya kuendelea kutekeleza sera ya ushirikishwaji Watanzania katika sekta ya Madini (Local Content) kwa ufanisi ili sekta hii inufaishe Watanzania wengi zaidi kutokana na uwekezaji wake kwa kuwa migodi ya Twiga- Barrick inazo fursa nyingi kwa ajili ya watanzania wazawa ili waweze kushiriki kwenye sekta ya madini.
Kutokana na utekelezaji wa sera hii kwa vitendo, migodi ya Barrick -Twiga ya North Mara na Bulyanhulu inashikilia rekodi ya kutunukiwa tuzo kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kutokana na kutambua mchango wake.
Kufikia mwaka jana, kampuni imetumia kiasi cha shilingi Tsh 1.2 trilioni kufanya manunuzi kwa wazabuni kutoka ndani ambayo ni sawa na asilimia 75% na ili kuhakikisha wazabuni wazawa wanaelewa taratibu za kufanya biashara na migodi yake ya Barrick imekuwa ikiendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo kupitia program yake ijulikanayo kama Local Business Development Program (LBDP) ambayo yamekuwa yakiendeshwa kwa wazabuni na wafanyabiashara mbalimbali kwa ajili ya kuwahamasisha kuchangamkia fursa za biashara zilizopo katika migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu.
Tangu Barrick ichukue usimamizi wa shughuli za madini mwaka 2019, kampuni imewekeza Dola za Kimarekani bilioni 4.79 katika uchumi wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na Dola milioni 558 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025 pekee. Zaidi ya asilimia 90 ya manunuzi yanaendelea kufanywa na wazabuni wa Kitanzania, wengi wao wakiwa kampuni za kizalendo, na asilimia 96 ya wafanyakazi ni Watanzania, huku asilimia 49 wakitoka katika jamii zinazozunguka migodi hiyo.


Post a Comment