VIJANA 100 WANG’ARA UCHUMI CHALLENGE, WABUNIFU WA TEHAMA WATAWALA

......

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Kamati ya Vijana Uchumi Challenge imetangaza rasmi majina ya vijana 100 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar waliofanikiwa kuingia hatua inayofuata ya shindano hilo linalolenga kukuza mawazo ya kibunifu na yanayotekelezeka kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu wa Kamati hiyo, Amina Sanga, amesema vijana hao wamepatikana baada ya ushindani mkubwa uliowakutanisha zaidi ya mawazo 7,852 yaliyowasilishwa na vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Amesema washiriki wengi wameonesha ubunifu mkubwa kupitia mawazo yao ambayo yanatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania, huku mawazo mengi yakijikita zaidi katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) pamoja na huduma za kidijitali.

“Tunawapongeza vijana wote walioshiriki kwa kuonesha uwezo mkubwa wa kufikiri na kubuni mawazo yenye kuleta mabadiliko chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu,” amesema Sanga.

Ameeleza kuwa dirisha la kupokea maombi lilifunguliwa mwezi Aprili mwaka huu na kupokea maoni mengi yenye ubunifu na tija, hali iliyoonesha mwitikio mkubwa wa vijana katika kushiriki maendeleo ya Taifa kupitia maarifa na teknolojia.

Kwa mujibu wa Sanga, hatua inayofuata itahusisha uchujaji wa vijana hao 100 ili kupata washiriki 30 watakaoingia hatua ya nusu fainali, kabla ya kupatikana washiriki 10 watakaoshindana katika fainali ya mashindano hayo.


Aidha, amesema washiriki wote 100 watapatiwa vyeti vya ushiriki kwa kutambua mchango wao, huku mshindi wa kwanza akitarajiwa kujinyakulia zawadi ya shilingi milioni 50 na mshindi wa pili kupata shilingi milioni 30.

Sanga amesema mchakato wa kuwachagua washiriki hao ulizingatia vigezo mbalimbali ikiwemo ubora wa mawazo, kiwango cha ubunifu, mchango wake katika uchumi wa Taifa pamoja na uwezekano wa mawazo hayo kutekelezwa kwa vitendo.

Katika hatua nyingine, amesema washiriki wote waliopita wataingia katika kambi maalumu ya mafunzo ya siku nne kuanzia tarehe 20 mwezi huu, ambapo watapatiwa mafunzo ya kitaalam yatakayowasaidia kuboresha mawazo yao na namna bora ya kuyawasilisha mbele ya majaji pamoja na wawekezaji.

“Washiriki wote mia moja wataingia kambini kukutana na wataalam mbalimbali watakaowasaidia kuboresha mawazo yao ili yaweze kuwa na tija zaidi katika jamii na uchumi wa Taifa,” amesema Sanga.
 

0/Post a Comment/Comments