Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam
WADAU wa sekta ya afya wameitaka serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kupunguza vikwazo vinavyoongeza gharama za utoaji huduma za afya, ikiwemo kodi na wingi wa mamlaka za udhibiti, ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kuboresha huduma kwa wananchi.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam wakati wa mjadala kuhusu ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) katika sekta ya afya ulioandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) kwa kushirikiana na wadau wa afya.
Mwekezaji katika sekta za afya na elimu, Dk. Mahmood Mringo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Hospitali Binafsi(APHFTA), alisema uwekezaji katika sekta ya afya unahitaji mtaji mkubwa lakini bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoongeza gharama za huduma.
Alisema pamoja na umuhimu wa sekta ya afya kwa ustawi wa wananchi, bado wawekezaji wanakabiliwa na kodi na mifumo ya udhibiti inayoongeza mzigo wa gharama katika utoaji wa huduma.
“Uwekezaji katika sekta ya afya ni wa gharama kubwa. Kama tunataka mabadiliko lazima tuangalie upya sera na mazingira yanayowezesha uwekezaji,” alisema.
Dk. Mringo pia alieleza kuwa gharama za huduma za afya nchini bado hazijulikani kwa usahihi kutokana na kukosekana kwa takwimu za kutosha za gharama halisi za utoaji wa huduma hizo, hali inayofanya kuwa vigumu kupanga bei na sera zinazolenga kupunguza gharama kwa wananchi.
Aidha, alishauri mamlaka za udhibiti zipunguzwe na kuwepo kwa mikakati ya kutafuta mitaji ya uwekezaji ili kuongeza uwezo wa sekta ya afya kukidhi mahitaji ya wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Viwanda vya Dawa Tanzania (TPMA), Bashiru Haroon, alisema sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na kwamba serikali inapaswa kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha wawekezaji kufanya kazi kwa ufanisi.
Alisema afya na elimu ni sekta muhimu zinazohitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi.
“Bila kuwa na wananchi wenye afya bora hatuwezi kufikia malengo ya maendeleo. Serikali na sekta binafsi lazima zishirikiane kwa karibu katika kuboresha huduma hizi,” alisema.
Aliongeza kuwa ni muhimu serikali kukaa pamoja na wadau wa sekta ya afya ili kupitia changamoto zinazowakabili wawekezaji, ikiwemo suala la kodi na gharama za uendeshaji wa huduma.
Akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wadau hao, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, alisema mfumo wa sheria za ubia tayari unatoa fursa mbalimbali za kuhamasisha uwekezaji katika miradi ya maendeleo.
Amesema kwa mujibu wa sheria serikali inaweza kushiriki kwa kutoa mtaji katika baadhi ya miradi ya ubia, kutoa misamaha ya kodi ili kupunguza gharama za uwekezaji pamoja na kutoa dhamana kwa miradi inayotekelezwa chini ya mfumo wa PPP.
Kafulila amesema msimamo wa serikali ni kuendelea kukuza na kuimarisha sekta binafsi kwa kuwa ni mshirika muhimu katika kufanikisha maendeleo ya taifa na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.


Post a Comment