📌 lengo ni kuimarisha uwajibikaji kwa wafanyakazi na kuboresha utendaji kazi
📌Kaimu katibu mkuu afungua rasmi mafunzo hayo na kuwataka watumishi kuzingatia mafunzo na maelekezo ya watoa mada.
Na Neema Mbuja, Dodoma
Kaimu katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Bwana Bernard Marcelline leo tarehe 9 Juni, 2026 amefungua rasmi mafunzo ya maadili ya utumishi wa umma, Afya ya akili pamoja na nidhamu ya fedha kwa wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii yenye lengo la kuwajengea uwezo wafanyakazi na kuboresha mazingira ya utendaji kazi
Bwana Marcelline amesema, mafunzo haya yana umuhimu wa kipekee kwa mfanyakazi mwenyewe na familia yake na jamii kwa ujumla, kwani changamoto hizi zimekuwa zikizorotesha utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma na kuwataka wafanyakazi kupambana nazo.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi msaidizi sehemu ya rasilimali watu Bi. Shani Kamala amesema, wameamua kuendesha mafunzo hayo kwa lengo la kukumbushana na kuwaelekeza wafanyakazi umuhimu wa maadili ya utendaji kazi kwenye utumishi wa umma ili kuleta mabadiliko.
Akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa maadili uwazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, Mkurugenzi wa elimu kwa umma kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa -TAKUKURU Bwana Joseph Mwaiswelo amesema ni vyema wafanyakazi kujiepusha na vitendo vinavyochochea mianya ya rushwa ili kuepuka usumbufu.
Amesema ni vema wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakaongozwa na utelekezaji wa majukumu yao unaozingatia maadili, uadilifu, uzalendo kama inavyoelekeza Dira na Dhima ya Wizara ili kuleta ufanisi kwenye utendaji kazi.
Amesema sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007 kifungu 15,22,31,33 vinamtaka mtumishi wa umma kujiepusha na hongo, matumizi mabaya ya mamlaka uliyonayo kwenye utendaji kazi na kutumia ushawishi kufanya ukuwadi na kuwataka watumishi wa umma kuzingatia haya.








Post a Comment