Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wananchi wametakiwa kuongeza umakini katika matumizi ya mitandao na huduma za kidigitali ili kujikinga dhidi ya vitendo vya utapeli wa mtandaoni, wizi wa taarifa binafsi na udikuzi wa mifumo, huku wakihimizwa kutafuta elimu sahihi ya usalama mtandao ili kuepuka hasara zinazoweza kujitokeza.
Hayo yalisemwa jijini Dodoma na Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kitengo cha Ulinzi na Usalama wa TEHAMA, Charles Liwongwe, wakati wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park.
Liwongwe alisema kitengo hicho kina jukumu la kuhakikisha mazingira ya kidigitali nchini yanakuwa salama, yenye kuaminika na yanayolinda maslahi mapana ya taifa pamoja na wananchi wanaotumia teknolojia za mawasiliano.
Alifafanua kuwa pamoja na kusimamia usalama wa mifumo ya TEHAMA, wizara imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi na salama ya mitandao ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoongezeka katika ulimwengu wa kidigitali.
“Tunatoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutumia mitandao kwa usalama, kutambua mbinu zinazotumiwa na matapeli wa mtandaoni na hatua za kuchukua pindi wanapokumbana na matukio ya uhalifu wa kidigitali,” alisema Liwongwe.
Aidha, aliwataka wananchi kutembelea banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika maonesho hayo ili kupata elimu na mwongozo wa matumizi salama ya teknolojia na huduma mbalimbali zinazotolewa na wizara.
Baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo wameeleza kufurahishwa na elimu wanayoipata, wakisema imewasaidia kuelewa zaidi namna ya kujilinda dhidi ya uhalifu wa mtandaoni.
Mkazi wa Dodoma, Peter Obogo, alisema amepata maarifa muhimu kuhusu usalama mtandao ambayo yameongeza uelewa wake baada ya kukumbana na matukio ya ujumbe wa kitapeli uliokuwa ukimtaka kutuma fedha kwenye namba zisizotambulika.
“Nilishawahi kukumbana na changamoto hiyo na karibu niwe mwathirika wa utapeli. Kupitia elimu niliyoipata hapa nimeelewa namna ya kutambua udanganyifu huo na hatua za kuripoti endapo tatizo litajitokeza,” alisema Obogo.
Alitoa wito kwa wananchi wengine kutembelea banda hilo ili kupata elimu itakayowasaidia kujikinga na changamoto za matumizi ya mitandao.
Kwa upande wake, mkazi mwingine wa Dodoma, Dayo Malando, alisema banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari limemuwezesha kupata uelewa mkubwa kuhusu huduma mbalimbali za kidigitali, hususan matumizi na umuhimu wa mfumo wa anwani za makazi.
Malando alisema kabla ya kutembelea banda hilo alikuwa akisikia kuhusu mfumo wa anwani za makazi bila kuelewa namna unavyofanya kazi, lakini sasa ameweza kufahamu jinsi ya kuutumia na faida zake katika kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Alieleza kuwa elimu inayotolewa na wizara ni muhimu kwa maendeleo ya jamii na itasaidia kuongeza uelewa kwa wananchi wengi zaidi kuhusu huduma za mawasiliano na teknolojia ya habari nchini.






Post a Comment