ZAIDI YA MIONGO SITA YA URAFIKI: TANZANIA NA SWEDEN ZAENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA MAENDE

******

Na Ashrack Miraji 

Mahusiano kati ya Tanzania na Sweden yanaendelea kuwa mfano wa ushirikiano wa muda mrefu uliojengwa katika misingi ya kuaminiana, kuheshimiana na dhamira ya pamoja ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Kwa zaidi ya miongo sita sasa, Sweden imeendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali muhimu zikiwemo elimu, afya, nishati, miundombinu, biashara na utafiti, huku ushirikiano huo ukizidi kupanuka kadiri mahitaji ya maendeleo yanavyobadilika.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias, alisema mahusiano ya nchi hizo mbili yamepiga hatua kubwa na yanaendelea kufungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii.

Alisema pamoja na historia ndefu ya ushirikiano wa maendeleo, sasa kuna msukumo mkubwa wa kuimarisha zaidi mahusiano ya kiuchumi kupitia biashara, uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi.

Kwa mujibu wa balozi huyo, kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Sweden kinaendelea kuongezeka ingawa bado hakijafikia uwezo halisi uliopo. Takwimu za mwaka 2024/2025 zinaonyesha Tanzania iliuza bidhaa nchini Sweden zenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni 3.9 huku bidhaa zilizoingizwa kutoka Sweden zikifikia dola milioni 68.

Hata hivyo, alisema takwimu hizo haziwezi kueleza kikamilifu ukubwa wa ushirikiano wa kiuchumi uliopo kati ya mataifa hayo mawili.

Moja ya maeneo yanayoonyesha ushirikiano huo ni utekelezaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), ambao umepewa msukumo mkubwa kupitia dhamana za mikopo zilizotolewa na taasisi ya Swedish Export Credit Agency (EKN).

Dhamana hizo zinazokaribia dola bilioni moja za Marekani kwa sehemu za kwanza hadi nne za mradi huo zinaonyesha namna Sweden inavyoendelea kuiamini Tanzania kama mshirika wa muda mrefu wa maendeleo na uwekezaji.

“Tunafurahishwa na mwelekeo wa sasa wa biashara. Tunaamini bado kuna nafasi kubwa ya kukuza mahusiano ya kiuchumi kati ya nchi zetu na kuona kampuni nyingi zaidi zikishirikiana katika siku zijazo,” alisema Balozi Ozaki.

Katika sekta ya elimu, Sweden imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Tanzania kupitia programu za kuimarisha ubora wa elimu, utafiti na ubunifu. Ushirikiano huo umehusisha pia miradi inayofadhiliwa kupitia Global Partnership for Education (GPE), ambayo imelenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza fursa za elimu kwa watoto kutoka makundi mbalimbali.

Balozi Ozaki alisema Sweden imefurahishwa na hatua ya Serikali ya Tanzania kuajiri takribani walimu 7,600 tangu mwaka 2023, hatua aliyoieleza kuwa muhimu katika kuimarisha ubora wa elimu na kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu.

Katika eneo la nishati, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuongeza upatikanaji wa umeme kwa wananchi wake, jambo ambalo limekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya watu.

Aliipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi zao za kupeleka huduma ya umeme katika maeneo mengi zaidi ya nchi.

Kwa upande wa miundombinu, balozi huyo alisema Tanzania inaendelea kujenga msingi imara wa maendeleo ya kiuchumi kupitia uwekezaji mkubwa katika barabara, madaraja, reli na mifumo mingine ya usafiri.

Aliitaja Dar es Salaam kuwa miongoni mwa miji inayokua kwa kasi zaidi duniani, jambo linaloakisi ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa shughuli za uwekezaji nchini.

Katika sekta ya afya, Balozi Ozaki alisema maendeleo yanayoonekana katika huduma za afya, hususan afya ya mama na mtoto, upanuzi wa vituo vya tiba na uwekezaji katika vifaa tiba, yanaonyesha dhamira ya Tanzania ya kuboresha ustawi wa wananchi wake.

Utalii nao ulipewa nafasi katika mazungumzo hayo, ambapo Balozi Ozaki aliielezea Tanzania kama moja ya nchi zenye vivutio vya kipekee zaidi duniani kutokana na urithi wake wa maliasili, wanyamapori, fukwe za Bahari ya Hindi na tamaduni zake mbalimbali.

Kwa sasa, takribani watalii 13,000 kutoka Sweden hutembelea Tanzania kila mwaka. Hata hivyo, alisema idadi hiyo inaweza kuongezeka zaidi ikiwa mazingira ya uwekezaji na ushindani katika sekta ya utalii yataendelea kuboreshwa.

Mbali na maendeleo ya kiuchumi, Balozi Ozaki aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa nguzo ya amani na utulivu katika ukanda wa Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla.

Alisema historia ya Tanzania katika kuunga mkono harakati za ukombozi wa nchi za Afrika pamoja na utamaduni wake wa kudumisha umoja wa kitaifa vimeifanya nchi hiyo kuheshimiwa kimataifa.

“Amani ni mtaji mkubwa wa maendeleo. Inatoa mazingira salama kwa uwekezaji, biashara na ustawi wa wananchi,” alisema.

Akiwa katika mwaka wake wa mwisho wa utumishi nchini Tanzania baada ya kuhudumu kwa miaka minne, Balozi Ozaki alisema ataondoka akiwa na kumbukumbu nyingi nzuri kuhusu maendeleo aliyoshuhudia pamoja na ukarimu wa Watanzania.


Aidha, maandalizi yanaendelea kwa maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Sweden yatakayofanyika Juni 6 mwaka huu nchini Sweden huku kupitia ubalozi wa Sweden nchini Tanzania ukiadhimisha siku hiyo Juni 4 mwaka huu. Siku hiyo huadhimisha matukio mawili muhimu katika historia ya Sweden; kuchaguliwa kwa Mfalme Gustav Vasa mwaka 1523 na kupitishwa kwa Katiba ya mwaka 1809, ambayo iliweka msingi wa maendeleo ya kidemokrasia ya taifa hilo.

Kwa zaidi ya miaka 60 ya ushirikiano, Tanzania na Sweden zinaendelea kuonyesha kuwa urafiki wa kweli kati ya mataifa unaweza kuwa chachu ya maendeleo, ustawi wa wananchi na kujenga mustakabali wenye manufaa kwa vizazi vijavyo.


 

0/Post a Comment/Comments