Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Urusi imefanikiwa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo kati ya Tanzania na Urusi katika maeneo tisa ya kimkakati yanayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi wa pande zote.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 7, 2026 jijini Dar es Salaam, Prof. Mkumbo alieleza kuwa Tanzania na Urusi zimeendelea kudumisha uhusiano wa kirafiki wa muda mrefu, huku ziara ya Rais Samia ikifungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika sekta mbalimbali muhimu.
Profesa Kitila alitaja maeneo ya ushirikiano kuwa ni pamoja na kilimo, elimu na mafunzo, nishati, madini, viwanda, usafiri, utalii, uchumi wa kidijitali, biashara na uwekezaji na kuongeza kuwa hatua za utekelezaji wa ushirikiano huo zimeanza kuzaa matunda, ambapo makubaliano kadhaa yalifikiwa kati ya taasisi za Tanzania na Urusi kwa lengo la kuimarisha mahusiano na kubadilishana utaalamu katika nyanja mbalimbali.
Alitaja makubaliano husika kuwa ni ushirikiano kati ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Chuo Kikuu cha MGIMO cha Urusi, unaolenga kuendeleza na kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Urusi ambapo Kiswahili kinatarajiwa kufundishwa kwa kiwango kikubwa zaidi katika taasisi za elimu nchini Urusi.
Profesa Kitila amesema katika mfumo wa kubadilishana tamaduni na lugha, lugha ya Kirusi pia inatarajiwa kuanza kufundishwa nchini na hivyo kuchangia kuimarisha mawasiliano, elimu na uhusiano wa watu wa mataifa hayo.






Post a Comment