ALEXIA SUPER CUP 2026 YAZINDULIWA KWA 'SHANGWE NA MATIBABU'

*********
Hospitali ya Alexia imetangaza kurejea kwa mashindano ya Alexia Super Cup msimu wa nne yatakayoanza Agosti 1, 2026, yakiambatana na huduma za afya bure kwa wananchi kupitia kaulimbiu ya "Shangwe na Matibabu."

Akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Alexia iliyopo Toangoma, Dar es Salaam, Operations Manager wa hospitali hiyo na Mratibu wa Alexia Super Cup, Anna Richard Msumule, amesema mashindano hayo ni sehemu ya mpango wa hospitali wa kurudisha kwa jamii kupitia burudani ya soka na huduma za afya.

Amesema msimu wa nne umeboreshwa kwa kuongeza huduma za afya, zawadi kwa washindi na ushiriki wa timu 16 kutoka Wilaya za Temeke, Kigamboni na Mkuranga.

Amefafanua kuwa uzinduzi utafanyika Agosti 1, 2026, ukianza na jogging na mazoezi ya viungo, kisha kambi ya matibabu, huku uzinduzi rasmi ukifanywa na Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Butchard Kakulu, kabla ya mechi ya ufunguzi kati ya Goroka na Tuwangoma City.

Operations Manager wa hospitali ya Alexia na Mratibu wa Alexia Super Cup, Anna Richard Msumule.

Akizungumza katika mkutano huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Alexia na Mratibu wa Kambi ya Matibabu, Dkt. Seif Salum, amesema wananchi watapatiwa huduma mbalimbali za afya bure katika Viwanja vya Masuliza kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

Amesema huduma zitakazotolewa ni pamoja na upimaji wa homa ya ini, sukari, shinikizo la damu, VVU, malaria, pamoja na uchunguzi na matibabu ya afya ya kinywa na meno na uchunguzi wa macho.

Dkt. Seif amesema huduma zote zitatolewa bila malipo, huku akibainisha kuwa kutakuwa pia na zoezi la uchangiaji damu litakalolenga kusaidia kuokoa maisha ya kina mama, watoto na wagonjwa wengine wanaohitaji damu.

Mratibu wa Kambi ya Matibabu, Dkt. Seif Salum, pamoja na Mratibu wa Alexia Super Cup, Anna Richard Msumule.

Anna amewaalika wananchi wa Tuwangoma, Mandege, Kisemvule, Vikindu, Kongowe, Vijibweni na maeneo mengine ya Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo, kupata huduma za afya bure na kushuhudia burudani mbalimbali, akisisitiza kuwa msimu huu utakuwa bora zaidi kuliko misimu iliyopita.


















.

0/Post a Comment/Comments