AYASOFIA HOTELS YAJIPANGA KUNUFAIKA NA AFCON 2027

.........

Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.

Kampuni ya hoteli za kifahari ya Ayasofia Hotels imejipanga kunufaika na ongezeko linalotarajiwa la watalii kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 (AFCON), ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza pamoja na Kenya na Uganda.

Kampuni hiyo imeonesha huduma na vivutio vyake vya utalii katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba, kwa kushirikiana na Tanzania Tourist Board na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Afisa Masoko wa Ayasofia Villas Dar es Salaam na Ayasofia Wildlife Arusha, Susan Kanje, amesema kampuni hiyo inaendelea na maandalizi ya kuwahudumia mashabiki wa soka pamoja na wageni wa kimataifa wanaotarajiwa kuingia nchini wakati wa mashindano hayo.

“Tupo hapa kuitangaza Ayasofia kama sehemu ya maandalizi ya AFCON 2027 na kuonesha uzoefu wa utalii ambao Tanzania inaweza kuwapatia wageni wa kimataifa,” amesema Kanje.

Amesema Ayasofia Villas Dar es Salaam, iliyopo Mbutu Beach, Kigamboni, ina majengo 29 ya malazi yanayowahudumia wageni binafsi, familia na makundi mbalimbali.

Mbali na malazi, hoteli hiyo ina huduma za ukumbi wa mikutano pamoja na maeneo ya wazi kwa ajili ya matukio ya kampuni, mafunzo ya pamoja ya wafanyakazi na shughuli nyingine za kijamii.

Kivutio kingine katika eneo hilo ni uwepo wa sehemu binafsi ya wanyamapori, yenye twiga, pundamilia, swala na mbuni, sambamba na wanyama wa aina adimu wakiwemo tiger wa Bengal na simba weupe.

Kwa upande wa Arusha, Ayasofia Wildlife Arusha iliyopo eneo la Maji ya Chai ndani ya Dolly Estate, inaunganisha malazi ya kifahari na uzoefu wa kuwatazama wanyamapori wanaozunguka kwa uhuru karibu na maeneo ya wageni.

Kanje amesema wageni wanaweza kuwaona baadhi ya wanyama moja kwa moja kutoka katika vyumba vyao, hali inayoongeza upekee wa huduma za hoteli hiyo.

Ameongeza kuwa eneo la hoteli hiyo kati ya Jiji la Arusha na Mount Kilimanjaro linatoa mandhari ya Mount Merupamoja na Mlima Kilimanjaro, jambo linalotarajiwa kuwavutia zaidi watalii wa kimataifa.

Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON 2027, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia maelfu ya wageni kutoka ndani na nje ya Afrika, huku yakichochea uwekezaji katika miundombinu ya michezo, usafiri na huduma za utalii katika nchi hizo tatu.



 

0/Post a Comment/Comments