******
BALOZI wa Tanzania nchini China, Dkt. Suleiman Haji Suleiman, amesema Serikali inaandaa mkakati maalumu wa kuwawezesha Watanzania kutumia kikamilifu soko la China kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.
Dkt. Suleiman amesema uamuzi huo umetokana na tathmini ya ushiriki wa Ubalozi wa Tanzania katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo zaidi ya Watanzania 500 walifika kupata taarifa kuhusu biashara na uwekezaji nchini China.
Amesema tathmini hiyo imebaini changamoto za uzalishaji mdogo, bidhaa kutokidhi viwango vya kimataifa, vifungashio visivyo na ushindani pamoja na uelewa mdogo wa taratibu za biashara za kimataifa.
Amesema ili kuondoa changamoto hizo, amependekeza kuanzishwa kwa Kliniki za Biashara zitakazowajengea uwezo wakulima na wafanyabiashara kuhusu uzalishaji, uchakataji, uongezaji thamani na namna ya kuingia katika masoko ya kimataifa.
Kadhalika, amesema kuna umuhimu wa kuanzishwa kwa Kituo cha Pamoja cha Biashara za Nje kitakachokusanya taasisi zote zinazotoa huduma za biashara mahali pamoja ili kurahisisha upatikanaji wa vibali, huduma za viwango, ushuru na usafirishaji wa bidhaa.
Wakati huohuo, Dkt. Suleiman amesema vijana wanaojaribu kupeleka dawa za kulevya nchini China hawatofanikiwa kutokana na ukali wa sheria za nchi hiyo, huku akionya kuwa adhabu zake ni kifungo cha maisha au kunyongwa.
Amesema kuna mzazi aliyefanya mazishi ya mwanawe akiamini amefariki nchini China, lakini baadaye ikabainika kuwa alikuwa amekamatwa kwa kosa la dawa za kulevya na anatumikia kifungo gerezani hadi mwaka 2031, akisisitiza vijana wajikite katika biashara halali na kutumia fursa zinazotokana na soko kubwa la China pamoja na sera ya ushuru sifuri kwa bidhaa kutoka Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, amesema mamlaka hiyo imeanza kuimarisha kituo cha pamoja cha kuwahudumia wafanyabiashara wanaolenga masoko ya kimataifa, hatua ambayo itarahisisha biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika soko la China.






Post a Comment