BARABARA YA TANGANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM, YAGEUKA KIVUTIO NA MGOGORO WA MIPAKA


 ....

Barabara ya Tanganyika iliyopo kati ya Kata ya Mbweni na Bunju, Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam, imegeuka kuwa kivutio kikubwa kutokana na umaarufu wa eneo hilo, ukuaji wa makazi na uwepo wa watu mbalimbali mashuhuri.

Eneo hilo limekuwa likivuta hisia za wananchi kutokana na uwepo wa makazi ya viongozi na watu maarufu, hali iliyosababisha baadhi ya wakazi kulitambulisha kwa jina la Mbweni kutokana na umaarufu wake unaoongezeka.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saady Mtambule, alifika katika eneo hilo kufuatilia suala la mpaka baina ya Serikali ya Mtaa wa Malindi Estate, Kata ya Mbweni, na maeneo yanayopakana na Kata ya Bunju.

Baadhi ya wakazi wamelielezea eneo hilo kama sehemu yenye mvuto mkubwa kutokana na maendeleo yanayoendelea, mazingira ya makazi pamoja na uwepo wa taasisi mbalimbali.

Mwenyekiti wa wenyeviti wa mitaa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Dovya, Anosisye Mwakiposa maarufu kama “Zimwi”, amesema historia ya eneo hilo inatokana na hatua za serikali za upimaji na upangaji wa maeneo.

Amesema kabla ya usajili rasmi wa baadhi ya mitaa, wananchi walikuwa tayari wameanza kutumia majina ya maeneo kwa mazoea kulingana na maeneo waliyokuwa wakiishi.

Kwa mujibu wa Zimwi, Mtaa wa Dovya ulitambuliwa na kuanzishwa mwaka 2004, huku Mtaa wa Malindi Estate ulipimwa na kusajiliwa rasmi mwaka 2014.

Ameeleza kuwa jina la Mbweni limeendelea kupata umaarufu kutokana na uwepo wa maeneo muhimu kama eneo la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambalo limekuwa sehemu ya kuitangaza zaidi sehemu hiyo.

Pia ametaja uwepo wa uwanja wa Isamuhyo unaotumika kwa shughuli za michezo, pamoja na uwepo wa kambi ya Simba SC katika Mtaa wa Malindi Estate kuwa miongoni mwa mambo yaliyoongeza umaarufu wa eneo hilo.

Mbweni pia imeendelea kujulikana kupitia uwepo wa timu za mpira wa miguu kama JKT Queens na Simba Queens, ambazo zimekuwa sehemu ya historia ya michezo katika eneo hilo.

Hata hivyo, ukuaji wa umaarufu wa Mbweni umeibua pia mjadala kuhusu mipaka ya maeneo kati ya mitaa inayopakana, huku viongozi wakihitajika kuweka wazi mipaka ya kiutawala ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi.

Kwa sasa, Mbweni imeendelea kuwa moja ya maeneo yanayokua kwa kasi jijini Dar es Salaam, likiwa na mchanganyiko wa historia, Barabara za kisasa, makazi ya kisasa, shughuli za kijamii na fursa mbalimbali za maendeleo.

0/Post a Comment/Comments