******
Na. OWM -TAMISEMI, Ulanga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha huduma za afya msingi kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya, ambapo Shilingi Bilioni 1.25 zimetolewa kuboresha utoaji wa huduma katika Hospitali ya Mahenge, wilayani Ulanga.
Prof. Shemdoe amesema hayo Julai 4, 2026, wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukagua na kuhimiza uwajibikaji alipotembelea hospitali ya Mahenge.
Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa, Serikali imedhamiria kuendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kuwezesha ujenzi wa miundombinu bora itakayorahisisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Prof. Shemdoe amesema fedha hizo zilizoidhinishwa na kutolewa na Mhe. Rais zitatumika kujenga jengo la huduma za dharura, wodi ya wazazi, kliniki ya watoto pamoja na uzio wa hospitali utakaoimarisha usalama wa wananchi wanaofuata huduma na kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Mhe. Salim Alaudin, amesema uboreshaji wa Hospitali ya Mahenge utawanufaisha wananchi wa Ulanga ambao hapo awali walilazimika kufuata huduma za dharura katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, hali iliyokuwa ikisababisha adha kubwa kwa wananchi na kusababisha vifo vya baadhi ya wagonjwa.
Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe pia ametembelea, amekagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 11, ukiwepo mradi wa ujenzi wa Daraja la Mbuga linalogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 2.35, ambalo linaunganisha barabara ya Mwaya, Iputi na Luhumbero.











Post a Comment