BODI YA FILAMU YAIPONGEZA CAC KWA KUUNGANISHA SANAA, YAHAMASISHA USAJILI WA WADAU

....

Na Carlos Claudio, Dodoma

Bodi ya Filamu Tanzania imeipongeza Chamwino Arts Centre (CAC) kwa kuendelea kuandaa Tamasha la Muziki wa Cigogo, ikieleza kuwa tamasha hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wadau wa sanaa mbalimbali na kufungua fursa za maendeleo kwa wasanii nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Chamwino Arts Centre, Dodoma, kuelekea ufunguzi wa Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo unaotarajiwa kufanyika kesho Julai 25, 2026, Afisa Maendeleo wa Bodi ya Filamu Tanzania, Ally Makata, alisema ushiriki wa bodi hiyo katika tamasha hilo unatokana na uhusiano mkubwa uliopo kati ya muziki na filamu.

Makata alisema watu wengi hujiuliza kwa nini Bodi ya Filamu inashiriki katika tamasha la muziki, lakini ukweli ni kwamba muziki ni sehemu muhimu ya filamu kwani huongeza ladha, hisia na mvuto kwa mtazamaji kupitia background music.

"Ndiyo maana leo Bodi ya Filamu tumeamua kuja Chamwino kwenye Tamasha la Cigogo Music Festival kushiriki pamoja na wadau wa sanaa. Hili ni jukwaa muhimu linalotuwezesha kukutana na wadau wetu mbalimbali," alisema.

Alieleza kuwa tamasha hilo linawakutanisha waigizaji, waendeshaji wa kamera, waongozaji wa filamu, watayarishaji pamoja na wanamuziki, huku akibainisha kuwa msanii anaweza kuwa na vipaji zaidi ya kimoja vinavyohitaji kutambuliwa na kuendelezwa.

Makata alisema kupitia tamasha hilo, Bodi ya Filamu inalenga kutoa elimu kuhusu fursa zinazopatikana serikalini kwa wadau wa filamu pamoja na kusajili wasanii ili watambulike rasmi na kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na bodi hiyo.

"Tupo hapa kuwaeleza wadau kuhusu fursa zilizopo serikalini kupitia Bodi ya Filamu, lakini pia tunawasajili ili waweze kutambulika rasmi na kuendeleza taaluma zao," alisema.

Aidha, aliipongeza Chamwino Arts Centre kwa kuandaa tamasha hilo ambalo limekuwa likiwakusanya Watanzania kutoka maeneo mbalimbali na kukuza sekta ya sanaa.

"Hakuna sanaa inayoweza kukosa muziki. Tunawapongeza Chamwino Arts Centre kwa juhudi zao za kuwakutanisha Watanzania kupitia sanaa. Hili ni jambo la kipekee na linapaswa kuigwa na wadau wengine nchini," alisisitiza.

 

0/Post a Comment/Comments