Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Mbelwa Kairuki, amekutana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, kujadili namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kati ya Tanzania, Uingereza na Ireland, kwa lengo la kuimarisha uwekezaji na kuwezesha biashara.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Julai 15, 2026 katika Ubalozi wa Tanzania uliopo jijini London Uingereza, viongozi hao wamejadili kwa kina kuhusu hatua za kutatua changamoto za walipakodi kutoka Uingereza waliopo Tanzania, ikiwemo kuboresha mazingira ya kikodi, kuondoa vikwazo visivyo vya lazima na kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma za kodi ili kuvutia na kudumisha uwekezaji endelevu.
Aidha, wamezungumzia umuhimu wa kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Tanzania kwenda Uingereza, ambapo wameainisha haja ya kuboresha mifumo ya forodha, kuongeza ufanisi wa bandari na kupunguza muda wa usafirishaji ili kuwezesha biashara kufanyika kwa haraka na gharama nafuu.
Vilevile, wamekubaliana juu ya umuhimu wa kuwa na afisa maalum (dedicated officer) ndani ya TRA atakayeshughulikia moja kwa moja changamoto za wafanyabiashara kutoka Uingereza na Ireland, hatua itakayosaidia kuongeza kasi ya utatuzi wa changamoto na kuboresha mawasiliano kati ya pande husika.


Post a Comment