Na HERI SHAABAN (ILALA
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametangaza msako mkali dhidi ya madanguro na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia mtu yeyote anayehusika na biashara hizo au kuwatumia watoto katika vitendo vya unyanyasaji.
Mpogolo aliyasema hayo Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wananchi, kata Zingiziwa katika kikao cha kutatua kero za wananchi
"Natangaza msako mkali dhidi ya madanguro na vitendo vya ukiukwaji wa maadili Serikali aitavumilia mtu yoyote anayefanya biashara hizo au kutumia watoto katika vitendo vya unyanyasaji"amesema Mpogolo.
Mkuu wa Wilaya Edward Mpogolo amesema taarifa zilizopo katika Kata ya Zingiziwa kulikuwa na mtu anayeshukiwa kuwatumia watoto wa kike kuwachezesha wakiwa uchi kwa malipo ya kati ya Shilingi 3,000 na 5,000, jambo alilosema ni ukatili mkubwa na ukiukwaji wa maadili ya jamii.
Mpogolo amesema mtuhumiwa huyo tayari amekamatwa na Jeshi la Polisi, huku wakiendelea na uchunguzi upelelezi ukikamilika atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Alitumia fursa hiyo kuwapongeza sana Jeshi la Polisi kwa umakini wa kwa kuchukua hatua mapema kabla madhara hayajaongezeka.
Aidha, aliwataka wenyeviti wa mitaa na wananchi kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola ili kuhakikisha madanguro yanatokomezwa, akisisitiza kuwa hakuna nafasi ya biashara zinazoharibu maadili na kuhatarisha usalama wa watoto na familia.
Mpogolo amesema umaskini hauwezi kuwa kisingizio cha kuwahusisha watoto au wanawake katika vitendo vinavyodhalilisha utu wa binadamu, akionya kuwa jamii ikivifumbia macho vitendo hivyo itakuwa inahatarisha mustakabali wa kizazi kijacho.
Pia aliwahimiza viongozi wa dini na jamii kuendelea kusimamia maadili mema, haiwezekani kupinga maovu makanisani na misikitini huku yakiachwa yaendelee katika maeneo ya makazi.
Wakati huo huo, aliipongeza Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) kwa operesheni zilizofanyika hivi karibuni, akieleza kuwa zaidi ya watu 20 walikamatwa katika msako dhidi ya vitendo hivyo.
Alisema operesheni hizo ni sehemu ya jitihada za kurejesha maadili, kulinda watoto na kuimarisha usalama wa wananchi katika Wilaya ya Ilala.






Post a Comment