Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, leo Julai 20, 2026 amekutana na Menejimenti na watumishi wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika Makao Makuu ya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, kwa kikao cha kutathmini utekelezaji wa shughuli za mwaka wa fedha uliopita na kuweka mikakati ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Dkt. Abbasi, ambaye amepokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, amesema Makumbusho ya Taifa ni taasisi muhimu yenye jukumu la kuhifadhi historia, utamaduni na urithi wa Taifa, huku akisisitiza kuwa mchango wa sekta hiyo unapaswa kuonekana katika maendeleo ya nchi.
"Sekta hii ina mchango wake kwa jamii, siasa na uchumi, na mchango huo unatakiwa uonekane. Misingi imara inatakiwa kuwekwa ili taasisi iweze kutimiza wajibu wake kwa ufanisi," amesema Dkt. Abbasi.
Amesema ni muhimu kuimarisha misingi ya taasisi kwa kuweka mikakati endelevu ya kuongeza mapato na kushirikisha wadau katika shughuli za kuhifadhi na kuendeleza urithi wa Taifa.
Aidha, amekielekeza Kitengo cha Masoko na Uhusiano kuandaa programu mbalimbali za masoko na utangazaji zitakazoongeza mwonekano wa Makumbusho ya Taifa, kuvutia wageni wengi zaidi na kuongeza mapato ya taasisi.
Dkt. Abbasi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Makumbusho ya Taifa kwa kutoa ushirikiano na msaada unaohitajika ili kuboresha huduma, kuimarisha uhifadhi wa urithi wa Taifa na kuongeza mchango wa taasisi hiyo katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga ametumia fursa hiyo
kusema kuwa Makumbusho itaendelea kufanya tafiti,kuihifadhi na kuielimisha
jamii kuhusu urithi wa utamaduni.
Baada ya kikao hicho,
Katibu Mkuu ametembelea onesho la kudumu la ndege ya kwanza ya Rais wa Kwanza
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
ambapo alielekeza kufanyika maboresho zaidi ya eneo hilo ili wageni wapate
fursa bora ya kujifunza historia ya chombo hicho cha kipekee na nafasi yake
katika historia ya Taifa hasa tunapoelekea katika mashindano ya AFCON 2027.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)




.jpeg)

.jpeg)


Post a Comment