WANAOJITOLEA KWENYE PROGRAMU YA JICA (JOCV) WASHIRIKI MAONESHO YA SABASABA

***** 

Dar es Salaam. 

Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) linaendelea kuwawezesha wanawake kujiongezea kipato kupitia utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwa urahisi na vifaa vinavyorejelewa.

Mpango huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya huduma za kujitolea za JICA nchini Tanzania.

Katika Maonesho ya 50  ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), washirika wa JICA wameonesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na vikundi vya wanawake.

Bidhaa hizo ni pamoja na sabuni za mikono, mapambo ya nywele yaliyosokotwa kwa uzi na hereni zinazotengenezwa kwa vifuniko vya chupa za plastiki vilivyorejelewa.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Aisha Lugendo, amesema wanawake hao walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali yaliyowawezesha kutumia uzi, sindano na plastiki kutengeneza bidhaa zenye thamani ya kibiashara.

Amesema zaidi ya wanawake 20 walipata mafunzo mwanzoni mwa mradi huo, huku 10 wakiendelea na uzalishaji wa bidhaa hizo na kujipatia kipato.

Amesema bidhaa hizo zimekuwa zikipata soko, lakini changamoto kubwa inayowakabili bado ni ukosefu wa masoko ya kudumu.

Lugendo amesema ushiriki wao katika Maonesho ya Sabasaba mwaka huu unalenga kutangaza bidhaa hizo, kupanua masoko na kuongeza kipato cha wanawake wanaoshiriki katika mradi huo.




0/Post a Comment/Comments