*****
DAR ES SALAAM
Tanzania ikiwa siku yake ya kwanza ya utekelezaji wa Dira 2050 leo tarehe 1, Julai, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), Mhe. David Kafulila, amesema Tanzania inaingia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiwa na msingi imara wa ukuaji wa uchumi, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi wa mashirika ya umma na kupanua wigo wa ukusanyaji wa kodi.
Kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), Kafulila amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa ya miaka 25 iliyoanza mwaka 2000/2001 inahitimishwa wakati uchumi wa Tanzania umeongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 13 hadi kufikia dola bilioni 94 mwaka 2025/26.
Amesema katika kipindi hicho, thamani ya jumla ya uzalishaji wa bidhaa na huduma nchini imefikia takribani dola trilioni 1.15, huku Dira 2050 ikilenga kufikisha uchumi wa Tanzania katika kiwango cha dola trilioni moja kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.
Kafulila ameeleza kuwa ili kufanikisha lengo hilo, ni muhimu mashirika ya umma yafanyiwe mageuzi ikiwemo kuorodheshwa katika soko la mitaji, hatua ambayo itaongeza upatikanaji wa mitaji kutoka sekta binafsi pamoja na kuimarisha uwajibikaji na ufanisi wa mashirika hayo.
Ameongeza kuwa mfumo huo umechangia mafanikio ya China kupitia sera ya Corporatization of Public Enterprises, inayolenga kuyafanya mashirika ya umma kufanya kazi kwa ufanisi unaofanana na ule wa sekta binafsi.
Aidha, Kafulila amesema sekta isiyo rasmi bado ni changamoto katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, akieleza kuwa kwa wastani Tanzania imekuwa ikikusanya kodi inayolingana na asilimia 12 ya uchumi kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita, kiwango kilicho chini ya wastani wa asilimia 15 wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Amesema kama Tanzania ingefikia kiwango hicho cha wastani, ingeweza kukusanya mapato ya ziada ya takribani dola bilioni 40, fedha ambazo zingetosha kugharamia ujenzi wa miradi mikubwa ya reli ikiwemo SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma, reli ya Mtwara–Mbamba Bay pamoja na reli ya Tanga–Musoma.
Kwa mujibu wa Kafulila, Serikali inalenga kuongeza uwiano wa mapato ya kodi kufikia asilimia 18 ya uchumi ifikapo mwaka 2030, kiwango kitakachozidi wastani wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na bara la Afrika kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa licha ya changamoto zilizopo, Tanzania ipo kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.





Post a Comment