KAMISHNA KANDA YA DAR ES SALAAM NA MKUU WA WILAYA KINONDONI KUHUDHURIA KESI ZA MIGOGORO YA ARDHI

........


Akizungumza na Radio UFM leo asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saady Mtambule, amewataka wakazi wa Kinondoni kutumia fursa ya Ardhi Clinic inayotarajiwa kufanyika katika eneo la Kulindima, Nyakasangwe, ili kuwasilisha changamoto zao za masuala ya ardhi na kupata suluhisho.

Mtambule amesema katika kliniki hiyo atakuwepo pia kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi pamoja na viongozi wengine, kwa lengo la kusaidia kutatua na kupunguza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo katika maeneo mbalimbali.

Amesema badala ya wananchi kutumia muda mwingi kugombania maeneo, wanapaswa kutumia njia za kisheria na kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha maendeleo yanaendelea.

“Wananchi wanapaswa kufika kwenye Ardhi Clinic ili matatizo yao ya ardhi katika mitaa yao yaweze kufanyiwa kazi. Migogoro mingi ikitatuliwa kwa wakati itaongeza kasi ya maendeleo,” amesema Mtambule.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuhusu utaratibu wa wananchi kushiriki katika kupaka rangi na kuboresha nyumba zao, akisema ni utaratibu uliowekwa kisheria tangu mwaka 1968 wenye lengo la kuboresha mazingira ya makazi.

Ameongeza kuwa kupaka rangi nyumba, ofisi na maeneo mbalimbali husaidia kuongeza uzuri wa miji, kuboresha mazingira na kuifanya Kinondoni kuwa eneo lenye mandhari bora.

Wananchi wa Kinondoni wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye Ardhi Clinic ili kupata huduma na ushauri kuhusu masuala ya umiliki wa ardhi, mipaka na migogoro mbalimbali


 

0/Post a Comment/Comments