.......
NA: DK. REUBENI LUMBAGALA
Mwelekeo wa serikali ni kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua kubwa za kimaendeleo kupitia sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo sekta ya viwanda.
Viwanda ni miongoni mwa nyenzo muhimu kufikia matarajio ya serikali ya kukuza uchumi na maendeleo ya nchi. Viwanda vina mnyororo mkubwa wa thamani ambapo mafanikio yake yanawezesha ukuaji wa sekta nyingine muhimu za kijamii na kiuchumi ili kukuza maendeleo.
Mipango ya serikali ni kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kongani za viwanda ili kuhakikisha ukuaji uchumi unakuwa jumuishi katika maeneo yote ya nchi.
Katika wilaya ya Pangani mkoani Tanga, upo mradi wa mashamba makubwa ya miwa pamoja na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari.
Mradi huo ni mpango wa serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kukuza uchumi na kuchochea ukuaji wa maendeleo.
Februari 26, 2025, akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Pangani, Rais Dk. Samia alieleza dhamira ya serikali ya kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa ya miwa na kujenga kiwanda cha sukari ili kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, ajira na kuurejesha mkoa wa Tanga katika sifa yake ya kuwa na maendeleo ya viwanda.
Aidha, mradi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ambapo katika mwezi Juni, 2026, zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wapatao 474 kutoka vijiji vya Mseko na Kigurusimba, Kata ya Masaika wilayani humo, limeanza.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani, amepongeza zoezi hilo la ulipaji fidia wananchi kwani ni hatua nzuri kuelekea utekelezaji wa mradi huo ambao una tija kubwa katika kukuza maendeleo ya mkoa wa Tanga na taifa kwa ujumla.
"Tayari zaidi ya wananchi 400 wameshakamilisha kusaini nyaraka zinazohitajika. Wale waliojitokeza mapema watapewa kipaumbele, huku wengine wakiendelea kuhudumiwa kadri zoezi linavyoendelea," amesema Balozi Dk. Buriani.
Kimsingi, mradi huo utagharimu dola za kimarekani milioni 350, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 900 za Kitanzania, huku ekari 22,000 zikitarajiwa kutumika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kabambe wilayani Pangani.
Kwahiyo, utekelezaji wa mradi huu utasaidia kuongeza fursa za ajira nchini hasa kwa vijana huku ukichangia uzalishaji wa sukari kwani dhamira ya serikali ni kuhakikisha nchi yetu inajitosheleza kwa mahitaji ya sukari na kuuza ziada nje ya nchi.
Pia, sekta ya kilimo wilayani Pangani itakua kwani wakulima wataongeza kasi ya uzalishaji wa miwa kutokana na uhakika wa soko katika kiwanda hicho.
Sambamba na hilo, mapato ya ndani wilayani humo pamoja na ongezeko la makusanyo ya kodi yataongezeka kupitia uwepo wa mradi huo. Haya yote yatachechemua uchumi na maendeleo ya wilaya ya Pangani, mkoa wa Tanga na taifa kwa ujumla.



Post a Comment