LATRA, COTWU WAANZISHA KAMPENI YA AFYA YA AKILI KWA MADEREVA KUPUNGUZA AJALI


 *****

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU), imeanza kampeni ya wiki ya kuhamasisha afya ya akili kwa madereva, ikisema hatua hiyo inalenga kupunguza ajali zinazochangiwa na msongo wa mawazo na uchovu kazini.

Kampeni hiyo inayofanyika katika maadhimisho ya Safer Action Week inalenga kuwafikia madereva wasiopungua 500 mkoani Dar es Salaam kabla ya kuendelea mkoani Mbeya.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa LATRA, Augustus Fungo, alisema madereva wanahitaji muda wa kutosha wa kupumzika kabla na wakati wa safari ili kuepusha uchovu unaoweza kusababisha ajali.

Alisema kwa safari zinazozidi saa nane, masharti ya leseni za usafirishaji yanataka kila basi kuwa na madereva wawili watakaopokezana kuendesha, huku akiwataka waajiri kuzingatia kikamilifu utaratibu huo.

Afisa Elimu Msaidizi wa COTWU, Nice Amoni, alisema afya ya akili imekuwa changamoto inayoongezeka kwa madereva kutokana na mazingira magumu ya kazi, foleni, miundombinu isiyoridhisha na changamoto nyingine zinazopunguza umakini wao barabarani.

Alisema kampeni hiyo pia inalenga kuwahamasisha waajiri kuboresha maslahi ya madereva kwa kuhakikisha wanalipwa stahiki zao kwa wakati, wanapatiwa bima ya afya, wanajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na kufanya kazi katika mazingira salama.

Amoni alisema madereva walioshiriki kampeni hiyo pia walipendekeza baadhi ya makosa ya usalama barabarani yatolewe maonyo badala ya adhabu kali pale inapowezekana.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), James Richard, alisema waendeshaji wa mabasi wanaendelea kutekeleza masharti ya LATRA yanayotaka safari za zaidi ya saa nane kuwa na madereva wawili.

Alisema TABOA imekuwa ikishirikiana na LATRA kuhakikisha mabasi ya masafa marefu yanazingatia utaratibu huo ili madereva wapate muda wa kupumzika na kupunguza ajali zinazotokana na uchovu.

Naye mwakilishi wa Wizara ya Uchukuzi alisema serikali inaendelea kushirikiana na LATRA kuandaa kanuni za kudhibiti uchovu wa madereva, akisisitiza kuwa ushirikiano wa serikali, waajiri na madereva ni msingi wa kuimarisha usalama wa usafiri na kulinda maisha ya watumiaji wa barabara.


0/Post a Comment/Comments