Na Carlos Claudio, Chamwino.
Sanaa ya uchoraji wa nyumba za tembe, iliyokuwa sehemu muhimu ya utambulisho wa jamii ya Wagogo lakini ikaanza kutoweka kutokana na mabadiliko ya makazi na maisha, sasa imeanza kufufuliwa kupitia mradi wa Mama Tembe, unaolenga kuhifadhi urithi wa utamaduni huku ukiwawezesha wanawake na wasichana kujipatia kipato kupitia ubunifu wa asili.
Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Innovation Development for Future Generation (IDFG) kwa ufadhili wa Serikali za Uswisi na Norway kupitia programu ya Articipate, na unatarajiwa kudumu kwa miezi sita. Mradi unawahusisha wanawake wazee 15 wa jamii ya Wagogo watakaowarithisha mabinti 20 pamoja na wanafunzi kutoka shule tatu mbinu za uchoraji wa jadi kwa kutumia malighafi na zana za asili zilizokuwa zikitumika kupamba nyumba za tembe.
Akizindua mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Kaimu Mkurugenzi, Dkt. Sophia Nchimbi, alisema hatua hiyo inaendana na juhudi za Serikali za kuhifadhi urithi wa taifa na wakati huo huo kufungua fursa mpya za maendeleo kupitia sekta ya utamaduni.
Alisema uchoraji wa nyumba za tembe si mapambo ya kawaida, bali ni sehemu ya historia na utambulisho wa jamii ya Wagogo, hivyo kufufuliwa kwake kutasaidia kuitangaza Chamwino kama kitovu cha utalii wa utamaduni na kuongeza thamani ya kazi za ubunifu zinazofanywa na wananchi.
"Tunafungua ukurasa mpya wa kuhifadhi utamaduni wetu. Kupitia mradi huu, Chamwino itanufaika kwa kuitangaza historia yake, lakini pia wananchi watanufaika kiuchumi kupitia kazi za sanaa. Halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha mradi huu unafanikiwa," alisema Dkt. Nchimbi.
Aidha, aliwataka wanawake na mabinti watakaopata mafunzo hayo kuutumia ujuzi huo kama mtaji wa maisha badala ya kuuona kama shughuli ya muda mfupi, ili uweze kuwa chanzo cha kipato hata baada ya mradi kukamilika.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Chamwino, Jackson Kitija, alisema mradi huo umefika wakati muafaka kwani baadhi ya maarifa ya jadi yalikuwa yakielekea kupotea kutokana na wazee waliokuwa nayo kuendelea kuzeeka huku vijana wengi wakikosa nafasi ya kujifunza.
Alisema uchoraji wa nyumba za tembe ni sehemu ya urithi usiogusika wa taifa, hivyo kuwarithisha vijana maarifa hayo ni njia sahihi ya kuhakikisha historia na utamaduni wa Wagogo vinaendelea kuishi kwa vizazi vijavyo.
Naye Mkurugenzi wa IDFG, Victoria Mponda, alisema mradi wa Mama Tembe ulianzishwa baada ya utafiti kubaini kuwa wanawake wa Kigogo walikuwa na mchango mkubwa katika kuhifadhi utamaduni kupitia michoro waliyoifanya kwenye nyumba za tembe, lakini mchango huo haukuwa umetambuliwa wala kuhifadhiwa ipasavyo.
Alieleza kuwa zamani wanaume walijenga nyumba huku wanawake wakizipamba kwa michoro iliyobeba alama na maana mbalimbali za maisha ya jamii. Hata hivyo, kutokana na kupungua kwa nyumba za tembe, ujuzi huo ulianza kutoweka na kubaki katika simulizi za wazee.
Mponda alisema mradi huo hautatoa mafunzo pekee, bali pia utakusanya historia ya michoro hiyo, kufafanua maana ya kila mchoro na kuhifadhi taarifa zote kidigitali ili ziwe rejea kwa vizazi vijavyo.
Aliongeza kuwa hatua nyingine ni kuhakikisha ubunifu wa wanawake hao unalindwa kupitia usajili wa hati miliki, huku michoro hiyo ikitumika kutengeneza bidhaa mbalimbali zenye thamani ya kiuchumi, ikiwemo mavazi na bidhaa nyingine zitakazobeba utambulisho wa sanaa ya Wagogo.
"Tunataka wanawake hawa watambulike kama wabunifu wa sanaa hii. Tutahifadhi kazi zao kidigitali, tutazisajili kwa hati miliki na baadaye kuzigeuza kuwa bidhaa zitakazoweza kuuzwa. Hii itasaidia kulinda urithi wetu na wakati huo huo kuwapa wanawake fursa ya kujipatia kipato kupitia ubunifu wao," alisema.
Alibainisha kuwa changamoto kubwa mwanzoni mwa utekelezaji wa mradi ilikuwa kuwashawishi wanawake wazee kushiriki, kwani wengi hawakuamini kuwa ujuzi walioutumia kwa miaka mingi kupamba nyumba ungeweza kuwa chanzo cha mapato.
"Kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na wa kimila tuliwafikia na kuwajengea uelewa kuwa sanaa nayo ni uchumi. Leo wamekubali kurithisha maarifa yao kwa mabinti, jambo ambalo tunaamini litakuwa mwanzo wa kufufua sanaa iliyokuwa ikielekea kutoweka," alisema.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Esteli Chibaya (84), mkazi wa Chamwino, alisema amefurahishwa na hatua ya kupewa nafasi ya kurithisha ujuzi alioupata tangu akiwa msichana, akiamini kuwa vijana wataendelea kuuenzi utamaduni wa Wagogo badala ya kuuacha upotee.
"Tulikuwa tunachora nyumba kwa ajili ya kuzipamba bila kujua kuwa siku moja ujuzi huu ungekuwa sehemu ya maendeleo yetu. Leo nina furaha kuona watoto na wajukuu wetu wataurithi na kuutumia kujenga maisha yao," alisema.



Post a Comment