MAMLAKA YABAINI ENERGY DRINKS ZENYE KIAMBATA CHA BANGI

Kamishina Jenerali wa Mamlaka  ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo.
******

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imebaini vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) vyenye kemikali ya THC inayopatikana kwenye dawa za kulevya aina ya bangi vikisambazwa katika duka la Village Supermarket, jijini Dar es Salaam.

Kamishina Jenerali wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo, alisema jana Julai 2, 2026 kuwa bidhaa hizo ziligunduliwa baada ya uchunguzi uliofanywa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Katika operesheni hiyo, makopo 122 ya kinywaji chenye chapa ya TRIP, kila moja likiwa na ujazo wa mililita 250, yalikamatwa. Pia, watuhumiwa wawili, Syed Abdul Bast (43), raia wa Pakistan, na Dhirendra Kumar Gorodhan (45), Mtanzania mwenye asili ya Asia, walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Lyimo alisema THC ni kemikali inayopatikana kwenye bangi na inaweza kusababisha madhara mbalimbali, yakiwemo kuathiri afya ya akili, kubadilisha utendaji wa mfumo wa fahamu, kuchochea vitendo vya uhalifu na kuongeza hatari ya matumizi ya dawa nyingine za kulevya.

Kutokana na ugunduzi huo, alisema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na taasisi nyingine itafanya ukaguzi wa bidhaa katika maduka mbalimbali nchini ili kuhakikisha hazina viambata vya dawa za kulevya vinavyoweza kuhatarisha afya ya watumiaji.

Akijibu swali kuhusu bidhaa hizo, Lyimo alisema zimetengenezwa nje ya Tanzania na kuingizwa nchini kinyemela. Aliongeza kuwa lebo za bidhaa hizo hazikuonyesha uwepo wa kemikali ya THC, jambo lililofichua udanganyifu uliofanywa na waingizaji wake.







 

0/Post a Comment/Comments