MUHIMBILI KUBORESHA MFUMO WA MALIPO YA HUDUMA ZA AFYA

 

****

Na Aveline Kitomary 

Hospitali ya Taifa Muhimbili imeweka mikakati ya kuimarisha mfumo wa malipo ya huduma za afya kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuongeza uwazi na kupunguza malalamiko ya wananchi.

Hatua hiyo imejadiliwa katika kikao kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Dellilah Kimambo, kilicholenga kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuongeza ufanisi wa mfumo wa malipo.

Dk Magembe amesema matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kuboresha huduma za afya na kuelekeza uongozi wa Muhimbili kuendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha malipo, kupunguza muda wa kusubiri wagonjwa na kuondoa mianya ya udanganyifu.

Amesema wananchi wanapaswa kupata taarifa za malipo wanayotakiwa kufanya kupitia simu zao za mkononi kabla ya kulipa, hatua itakayoongeza uwazi na kuwapa fursa ya kuhakiki usahihi wa gharama za huduma wanazopokea.

“Mwananchi apate taarifa za malipo anayotakiwa kufanya kiganjani mwake kupitia simu ili kabla ya kulipa ajihakikishie kama malipo hayo ni sahihi au hapana,” amesema Dk Magembe.

Aidha, amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili kuimarisha usimamizi wa huduma kupitia wakurugenzi, mameneja na wasimamizi wa hospitali, huku akisisitiza hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watumishi wasiowajibika na masuala yanayohitaji uamuzi wa Wizara yawasilishwe kwa hatua zaidi.

Pamoja na hayo, Dk Magembe amepongeza maboresho yanayoendelea kufanyika hospitalini, akiwapongeza watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa kujituma na weledi, akisema juhudi hizo zinaendelea kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.





0/Post a Comment/Comments