MWAKIPOSA ATAKA USHIRIKIANO, ATOA KAULI KUHUSU MGOGORO WA MIPAKA DOVYA NA MALINDI ESTATE


............

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Manispaa ya Kinondoni, Razalosi Mwakiposa maarufu kama Zimwi, amewataka wenyeviti wa mitaa kujenga mshikamano, kushirikiana na kulinda heshima ya nafasi wanazoziongoza ili kuimarisha huduma kwa wananchi.

Akizungumza kuhusu wajibu wa viongozi wa serikali za mitaa, Mwakiposa amesema wananchi wa sasa wana uelewa mkubwa na wana uwezo wa kutambua viongozi wanaotekeleza majukumu yao kwa uadilifu na wale wasiowajibika ipasavyo.

Amesema mafanikio yake katika uongozi wa eneo la DOVYA yametokana na kuwa mkweli kwa wananchi na kutoa huduma bila kuwatoza fedha kinyume cha taratibu, jambo ambalo limejenga imani kubwa kwa wananchi wake.

Aidha, amesema viongozi wa mitaa wanatarajia kushiriki semina maalumu za kuwajengea uwezo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa weledi, kuimarisha maadili ya uongozi na kuondoa dhana ya ubaguzi wa wananchi kutokana na hali zao za kiuchumi.

Kuhusu mgogoro wa mipaka kati ya DOVYA na Kata ya Mbweni, Mwakiposa amesema historia inaonesha kuwa DOVYA ilianza mwaka 2004, huku Mtaa wa Malindi Estate ukianzishwa mwaka 2015 baada ya kuunganishwa kwa iliyokuwa mitaa ya Mbweni Malindi na JKT Mbweni.

Ameeleza kuwa mpango wa upimaji na upangaji wa maeneo ulifanywa na Wizara ya Ardhi kuanzia mwaka 2000, huku viwanja vikianza kuuzwa mwaka 2003 kwa kufuata taratibu rasmi za serikali.

Kwa mujibu wa Mwakiposa, suala la mpaka lilipatiwa ufumbuzi mwaka 2024 katika kikao kilichowashirikisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saady Mtambule, aliyekuwa Diwani Richie Mtambalike, viongozi wa serikali za mitaa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wataalamu wa mipango miji.

Amesema katika kikao hicho, ramani rasmi ilisomwa na kuonesha kuwa Barabara ya Tanganyika, inayojulikana pia kama Rogers, ndiyo mpaka unaotenganisha Kata za Mbweni na Bunju.

Kutokana na maelezo hayo, Mwakiposa amehoji sababu za kuendelea kujitokeza kwa migogoro ya mipaka ikiwa tayari kulikuwa na ufafanuzi wa kitaalamu na wa kiserikali, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuweka mbele maslahi ya wananchi, amani na maendeleo badala ya kuendeleza migogoro isiyo na tija.

Mwisho, ametoa wito kwa viongozi wote wa serikali za mitaa kuendelea kushirikiana, kuheshimu sheria na kutumia njia za mazungumzo katika kutatua changamoto zinazojitokeza kwa manufaa ya wananchi

0/Post a Comment/Comments