Dar es Salaam, Julai 17, 2026
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetangaza nafuu kwa waajiri wenye malimbikizo ya michango kwa kuwapatia fursa ya msamaha wa tozo zitokanazo na ucheleweshaji wa michango, huku ukiwataka kuchangamkia fursa hiyo ili kupunguza mzigo wa madeni, kuimarisha uzingatiaji wa sheria na kulinda haki za wafanyakazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema kuwa msamaha huo, ulioanza kutekelezwa tarehe 1 Juni 2026, utaendelea hadi 31 Desemba 2026.
Bw. Mshomba alieleza kuwa tangu kuanza kwa msamaha huo, waajiri wameonyesha mwitikio chanya ambapo hadi sasa zaidi ya waajiri 6,000 wamejitokeza kutumia fursa hiyo na Mfuko umekwishakusanya zaidi ya shilingi bilioni 46 za michango tangu kuanza kwa msamaha huo tarehe 1 Juni 2026.
“Tunawasihi waajiri wote kutumia fursa hii mapema. Fedha ambazo wangezilipa kama tozo wanaweza kuzielekeza katika shughuli za uzalishaji, upanuzi wa biashara, kuongeza tija na kuboresha ustawi wa wafanyakazi,” alisema Bw. Mshomba.
Alisema msamaha huo utaendelea hadi tarehe 31 Desemba 2026, ambapo waajiri watakaolipa malimbikizo yote ya michango ya msingi ifikapo tarehe 31 Agosti 2026 watanufaika na msamaha wa asilimia 100 ya tozo.
Alifafanua kuwa waajiri watakaokamilisha malipo yao kati ya Septemba na Oktoba 2026, watanufaika na msamaha wa asilimia 75, huku wale watakaolipa kati ya Novemba na Desemba 2026 wakipata msamaha wa asilimia 50.
Aidha, alisema waajiri ambao hawakuwa na malimbikizo ya michango hadi tarehe 31 Mei 2026 lakini walikuwa na tozo pekee, watanufaika na msamaha wa asilimia 100 endapo wataendelea kuwasilisha michango yao kwa wakati hadi mwezi Desemba 2026.
Bw. Mshomba alisema fursa hiyo imetolewa ili kuwapa waajiri nafasi ya kurekebisha hali ya ulipaji wa michango na kutumia fedha ambazo zingelipwa kama tozo katika shughuli za uzalishaji, kuongeza tija na kuboresha mazingira ya kazi.
“Fedha ambazo waajiri wamekuwa wakizilipa kwa ajili ya kufidia tozo zinaweza kuelekezwa katika kuboresha maeneo yao ya kazi, kuongeza tija na kuimarisha uzalishaji.
Ndiyo maana fursa hii imetolewa ili waajiri wanufaike,” alisema.
Alisema ulipaji wa michango kwa wakati ni muhimu kwa kuwa unamwezesha mfanyakazi kupata haki zake za hifadhi ya jamii wakati anapopata majanga mbalimbali ikiwemo kustaafu.
NSSF YAENDELEA KUIMARIKA
Katika hatua nyingine, Bw. Mshomba alisema NSSF imeendelea kuimarika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, ambapo thamani ya Mfuko imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.8 mwezi Machi 2021 hadi kufikia zaidi ya shilingi trilioni 11.6 Juni 2026.
Alisema ukuaji huo umechangiwa na ongezeko la wanachama na michango, uwekezaji wenye tija, mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma.
Alieleza kuwa kupitia mifumo ya TEHAMA, waajiri na wanachama sasa wanaweza kufuatilia na kuwasilisha michango, kufuatilia madai ya mafao na kupata huduma mbalimbali bila kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
Kuhusu ulipaji wa mafao, Bw. Mshomba alisema Mfuko umeendelea kuboresha mifumo yake ambapo kwa sasa mafao mengi hulipwa ndani ya siku 20, tofauti na siku 60 zinazotakiwa kisheria.
“Lengo letu ni kuhakikisha mwanachama anapata stahiki zake kwa wakati. Endapo kuna ucheleweshaji mara nyingi chanzo huwa ni mwajiri kutowasilisha michango kwa wakati,” alisema.
UWEKEZAJI WENYE TIJA, SKIMU YA HIFADHI KUONGEZA WANUFAIKA
Akizungumzia uwekezaji, alisema NSSF inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati inayochangia ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira, akitolea mfano Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi ambacho kimeendelea kuongeza uzalishaji, kutoa ajira na kuwawezesha wakulima wanaokizunguka.
Kuhusu Skimu ya Hifadhi, Bw. Mshomba alisema mpango huo umewezesha wananchi waliojiajiri kujiunga na mfumo wa hifadhi ya jamii na kunufaika na mafao mbalimbali ikiwemo pensheni ya uzee, pensheni ya ulemavu, pensheni ya urithi, mafao ya uzazi, msaada wa mazishi pamoja na huduma za matibabu.
“Tunawahimiza waliojiajiri kujiunga kupitia Skimu ya Hifadhi kwa sababu mpango huu unabadilisha maisha yao na kuwapa uhakika wa kunufaika na mafao mbalimbali. Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa Staa wa Mchezo katika kujilinda dhidi ya changamoto za maisha,” alisema Bw. Mshomba.
Alisema NSSF itaendelea kushirikiana na waajiri, wafanyakazi na wadau mbalimbali katika kuimarisha mfumo wa hifadhi ya jamii nchini na kuhakikisha unaleta manufaa kwa Watanzania wengi zaidi.

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

Post a Comment