NYATI: TAMASHA LA CIGOGO LIMETUPA JUKWAA LA KIMATAIFA

...........

Na Carlos Claudio, Dodoma

Katibu Mkuu wa Kikundi cha Muziki wa Asili wa Kigogo cha Nyati Mchoya, Yaledi Petro, amesema Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo limekuwa chachu ya kuwafungulia wasanii wa muziki wa asili milango ya fursa mbalimbali kwa kuwawezesha kujitangaza kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Yaledi amesema tamasha hilo limeongeza mwonekano wa wasanii wa muziki wa asili na kuwafanya kutambulika zaidi ndani na nje ya nchi, hali inayotarajiwa kuongeza mialiko ya kushiriki maonesho na matamasha pamoja na kutangaza utamaduni wa Kigogo kwa urahisi.

“Tamasha hili limetupa fursa kubwa ya kuonekana na kujulikana. Mara nyingi tunapokea taarifa kuwa tunaonekana kwenye televisheni na mitandao ya kijamii, jambo ambalo linatusaidia kupata utambulisho na kufungua fursa za kazi na mialiko mbalimbali,” amesema.

Aidha, ameipongeza Chamwino Arts Centre (CAC) kwa kuendelea kuandaa tamasha hilo, akizitaka taasisi za Serikali na sekta binafsi kuunga mkono juhudi hizo ili kuhakikisha matamasha ya utamaduni yanaendelea kufanyika na kuwainua wasanii wa muziki wa asili kiuchumi.

“Tunawaomba wadau mbalimbali waendelee kuunga mkono matamasha kama haya. Yana mchango mkubwa katika kuhifadhi utamaduni wetu na wakati huo huo yanawapatia wasanii kipato na fursa za kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Akizungumzia kikundi chao cha Nyati, Yaledi amesema wamejikita katika kuandaa kizazi kipya cha wasanii kwa kuanza kuwafundisha watoto tangu wakiwa shule za msingi hadi sekondari, ambapo wanajifunza kupiga rimba, kutumia ala za asili pamoja na kuimba na kucheza ngoma za Kigogo.

Amesema uwekezaji huo unalenga kuhakikisha utamaduni wa Kigogo unaendelea kurithishwa kwa vizazi vijavyo huku ukitoa nafasi kwa vijana kukuza vipaji vyao.

Kwa upande wa matarajio, amesema kupitia Tamasha la Cigogo wamekutana na wageni kutoka mataifa mbalimbali waliovutiwa na kazi zao, jambo analoamini litafungua milango ya ushirikiano na fursa za maonesho ndani na nje ya Tanzania.

Yalediameyasema hayo Julai 25, 2026, jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika hitimisho la Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo lililofanyika katika viwanja vya Chamwino Arts Centre (CAC).



 

0/Post a Comment/Comments