PROF. SHEMDOE AMSHUKURU RAIS SAMIA NA BARRICK KWA KUPELEKA TABASAMU MASHULENI

*******

Na OWM - TAMISEMI, Kibaigwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals kwa kupeleka tabasamu mashuleni kupitia majadiliano waliyoyafanya ambayo yalipelekea Barrick kuchangia zaidi ya shilingi bilioni 70 za kitanzania ambazo zimewezesha ujenzi wa madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika shule za sekondari 132 nchini. 

Prof. Shemdoe ametoa pongezi hizo kwa Mhe. Rais na Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals Julai 02, 2026 akiwa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaigwa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa miundombinu ya shule za kidato cha tano na sita, ambao unaofadhiliwa kupitia ushirikiano wa Serikali na Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals. 

“Nampongeza sana Mhe. Rais kwa kuwaona Barrick kama wadau muhimu, na nawashukuru na kuwapongeza Barrick kwa kuleta fedha za kuwekeza kwenye sekta hii muhimu ya elimu,” ameeleza Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, ni chini ya uongozi makini wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndipo yalipoanzishwa majadiliano kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick ya kuimarisha ushirikiano katika kuchangia maendeleo ya jamii kupitia uwekezaji wa sekta ya elimu, na kuongeza kuwa majadiliano hayo yalipelekea kupatikana kwa zaidi ya bilioni 70 za kitanzania ziloizotumika kwenye ujenzi wa madarasa, mabweni na matundu ya vyoo.

Aidha, Prof. Shemdoe ameelekeza kamati iliyoshiriki kwenye majadiliano ya awali ya mwaka 2023 na Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals kurejea tena kwenye majadiliano mengine na kampuni hiyo, ili awamu awamu ya pili ya mradi huo ikikamilika zipatikane fedha nyingine za kuendelea kujenga miundombinu bora ya elimu.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals Bi Penina Kituku ambaye ni Meneja wa Fedha amesema kuwa, uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 70 za kitanzania walioufanya una maana kubwa kwa jamii na unakwenda moja kwa moja kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, ikiwa ni pamoja kutoa fursa kwa wanafunzi kusoma katika mazingira bora na salama.

Naye, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia elimu Bw. Atupele Mwambene,amesema kwamba mradi huo ulianzishwa kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri ambao wanajiunga na kidato cha tano, na kuongeza kuwa afua ambazo zimetekelezwa nchi nzima mpaka hivi sasa ni ujenzi wa madarasa 1090, mabweni 270 na matundu ya vyoo 1640.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Kibaigwa, Bw. Alex Sailemi amesema kuwa, wakazi wa Kibaigwa wanayo sababu ya kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  pamoja na Kampuni ya Barrick kwa kujengewa miundominu ya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaigwa.










0/Post a Comment/Comments