JAFO ATOA WITO WA KUUNGA MKONO RAJAI FOUNDATION, APONGEZA UTOAJI WA HUDUMA KWA JAMII

....

Na Carlos Claudio, Dar es Salaam

Mbunge wa Kisarawe, Mhe. Selemani Jafo, ametoa wito kwa Watanzania na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi kuendelea kuunga mkono taasisi zinazojihusisha na shughuli za kijamii, akisema kufanya jambo moja la kheri kwa ajili ya jamii ni njia ya kupata neema na kuchangia maendeleo ya taifa.

Jafo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya Impact Gala iliyoandaliwa na Rajai Foundation kwa ajili ya uzinduzi wa Rajai TV.

Aliipongeza Rajai Foundation kwa kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, akitaja uchimbaji wa visima zaidi ya 175 kuwa moja ya mafanikio makubwa yaliyowezesha wananchi na mifugo kupata maji safi na salama.

"Kuchimba visima zaidi ya 175 si jambo dogo. Hii ni kazi kubwa ambayo imewanufaisha wanadamu na hata mifugo. Ni mfano wa huduma inayogusa maisha ya watu moja kwa moja," alisema Jafo.

Alisema utoaji wa chakula kwa wananchi wenye uhitaji ni hatua muhimu inayodhihirisha dhamira ya taasisi hiyo ya kuwahudumia walio katika mazingira magumu, huku akiipongeza pia kwa miradi mingine ya kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii.

Jafo alisema inatia moyo kuona Rajai Foundation iliyoanzia mkoani Singida sasa imepanua shughuli zake katika maeneo mengine ya nchi, jambo linaloonyesha ukuaji wa taasisi na kujitolea kwa vijana wanaoiendesha.

Aliwahimiza watu wenye uwezo wa kifedha na wadau wa maendeleo kujitokeza kuisaidia taasisi hiyo ili iweze kupanua zaidi huduma zake kwa wananchi.

"Kuna watu wengi wenye uwezo mkubwa wa kifedha. Naomba wajitokeze kuziunga mkono taasisi kama Rajai Foundation ambazo zimeonyesha dhamira ya kweli ya kuisaidia jamii," alisema.

Aidha, alieleza kufurahishwa na hatua ya kuanzishwa kwa Rajai TV, akisema chombo hicho kitasaidia kutoa elimu, taarifa na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Jafo alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano, uaminifu na ushirikiano miongoni mwa wadau wa maendeleo, akieleza kuwa misingi hiyo ndiyo itakayoiwezesha Rajai Foundation kufikia malengo yake.

Alisema ana imani kuwa endapo taasisi hiyo itaendelea kupata ushirikiano kutoka kwa wadau, ndani ya miaka miwili hadi mitatu inaweza kuwa miongoni mwa taasisi kubwa na zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii nchini.

"Watoto yatima na makundi mengine yaliyoguswa na huduma za Rajai Foundation watakuwa mashahidi wa mema yaliyofanywa na taasisi hii," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tuzo ya Mashindano ya Dunia ya Qur'an Tukufu, Sheikh Othman Kaporo, aliwataka Waumini wa Kiislamu kujenga utamaduni wa kutoa badala ya kusubiri kupokea.

Alisema dini inahimiza kusaidia jamii, na kwamba kujitoa kwa ajili ya wengine kunaleta baraka duniani na Akhera.

"Tumekuwa tukitaka kupewa kuliko kutoa. Ni wakati sasa wa kubadili mtazamo huo kwa kujitoa kusaidia jamii, kwani kufanya hivyo kunaleta kheri duniani na mbinguni," alisema Sheikh Kaporo.

0/Post a Comment/Comments