RASIMU YA MWONGOZO WA UANZISHAJI NA USIMAMIZI WA WMAs WAIVA

...........

Na Sixmund Begashe, Dodoma 

WIZARA ya Maliasili na Utalii, kupitia Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (TWPF) imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa Uanzishaji na Usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) ambao pamoja na mambo mengine, unalenga kuimarisha uendeshaji wa shughuli za jumuiya na utatuzi wa changamoto zinazozikabili jumuiya hizo nchini. 

Akifungua Kikao Kazi Shirikishi cha uandaaji wa Mwongozo huo, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, jijini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori Bi. Kay Kagaruki, amesema kuwa hatua hiyo ni utekekezaji wa maelekezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) katika kuboresha shughuli za uhifadhi kwa kushirikiana na jamii kupitia jumuiya hizo. 

"Serikali kupitia Wizara kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi imeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha jumuiya zinaendelea kuimarika kwa kutatua changamoto zinazokabili maeneo hayo," amesema Bi. Kagaruki.

Ameongeza kuwa ni vyema kila mwananchi akatambua kuwa ana wajibu na jukumu la kulinda na kuendeleza uhifadhi wa maliasili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mratibu wa Kikao Kazi hicho Bi. Rose Mndendemi amebainisha kuwa kwa sasa kuna jumla ya WMAs 24 zilizoidhinishwa na kupata haki ya matumizi ya rasilimali za wanyamapori na jumuiya 16 zipo katika hatua mbalimbali za kupata haki hiyo. 

Naye Afisa Wanyamapori Halmashauri ya Wilaya Babati, Bw. Christopher Laizer ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwashirikisha katika uandaaji wa rasimu hiyo, na kusema kuwa Muongozo huo utakapokamilika na kutumika utawawezesha kuzisimamia vyema jumuiya hizo kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kikao hicho cha siku tatu, kimehudhuriwa na Maafisa wa Wizara, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Maafisa Wanyamapori wa Wilaya na wadau wengine, pia kitahusisha viongozi wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori nchini.












 

0/Post a Comment/Comments