Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ameshiriki ibada ya kuuaga mwili wa Profesa Pius Paul Mbawala, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika na Mbunge wa Namtumbo, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Josefu Namabengo Wilayani Namtumbo.
Akizungumza baada ya ibada hiyo, Brig. Gen. Ahmed amesema Profesa Mbawala atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya wilaya ya Namtumbo, mkoa na taifa kwa ujumla. Akisisitiza kuwa Prof. Mbawala alionyesha uzalendo, uadilifu, hekima na kujitoa kupitia nafasi mbalimbali za uongozi alizoshika, ikiwemo ubunge na utumishi serikalini.
Amesema kifo chake ni pigo kubwa kwa familia, wananchi wa Ruvuma na taifa, lakini urithi wa mema aliyoyaacha utaendelea kuishi ikiwemo elimu, uongozi bora, uzalendo na huduma kwa jamii.
Katika hatua nyingine, RC Ahmed amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Mkurugenzi na watumishi wote kuhakikisha kituo cha afya cha Namabengo kinachojengwa kiitwe Kituo cha Afya Profesa Pius Mbawala, kama ilivyoombwa na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera.
Amesema kumbukumbu hiyo itakuwa ishara ya heshima kwa kazi njema alizozifanya marehemu, ambazo zitaendelea kuishi katika nyoyo za watu wa Ruvuma na Watanzania. Katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, RC Ahmed amewaombea wanafamilia nguvu, uvumilivu na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Namtumbo, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Profesa Mbawala alihimiza maendeleo ya ushirika na kilimo cha umwagiliaji, akisisitiza kuwa mchango wake ulileta mafanikio makubwa ikiwemo kuanzishwa kwa skimu ya umwagiliaji.
Profesa Pius Paul Mbawala alihudumu kama Mbunge wa Namtumbo kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, na katika kipindi hicho aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika kuanzia mwaka 1997 hadi 2000, kisha Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula kuanzia mwaka 2000 hadi 2005.



Post a Comment