ROBOTICS KUWA CHACHU YA KUWAWEZESHA WASICHANA KATIKA TEHAMA

..........

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Muhandisi Mwandamizi wa Mawasiliano kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Brian Kaduma, amesema elimu ya Robotics aliyoipata kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali itakuwa chachu ya kuwawezesha wasichana kuingia katika taaluma za TEHAMA pamoja na kuchochea matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta za uzalishaji nchini.

Akizungumza jijini Dodoma, Kaduma alisema anatarajia kutumia ujuzi huo katika programu mbalimbali zinazotekelezwa na UCSAF, hususan programu ya "Msichana katika TEHAMA", kwa kuwapatia wanafunzi wa kidato cha tatu maarifa ya msingi kuhusu Robotics ili kuwajengea hamasa ya kuipenda taaluma hiyo na kujipanga kuwa wataalamu wa baadaye katika sekta ya teknolojia.

"Ninategemea kupitia programu mbalimbali za UCSAF, kama vile Msichana katika TEHAMA, kuwapa wasichana nafasi ya kujifunza Robotics mapema. Hii itawasaidia kufurahia teknolojia na kujijengea msingi wa kuwa wabobezi wa TEHAMA katika siku zijazo," alisema Kaduma.

Alieleza kuwa amefanikiwa kupata Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Robotics kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, akibainisha kuwa taaluma hiyo inalenga kutumia teknolojia kuongeza ufanisi wa uzalishaji, hasa katika viwanda na shughuli za kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania ili ziweze kushindana katika soko la kimataifa.

Kaduma alisema dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwaandaa watumishi wa umma katika teknolojia zinazoibukia imezaa matunda, kwani elimu hiyo imemwezesha kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya kupata mafunzo hayo.

Aidha, alisema maarifa aliyopata yameongeza uwezo wake wa kutumia akili mnemba (Artificial Intelligence) na teknolojia nyingine za kisasa katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, sambamba na kuongeza uelewa wake wa kitaaluma katika sekta ya TEHAMA.

Kaduma aliongeza kuwa fursa ya kusoma nchini Uingereza haikumjengea tu uwezo wa kitaaluma, bali pia ilimpa nafasi ya kujifunza tamaduni mbalimbali na mifumo tofauti ya elimu, jambo ambalo limepanua mtazamo wake kuhusu maendeleo ya teknolojia duniani.

Alisema malengo yake ya baadaye ni kuendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Robotics ili kuwa mtaalamu bingwa katika eneo hilo, huku akisisitiza kuwa kwa sasa anajikita katika kushirikisha maarifa aliyoyapata na watumishi wenzake pamoja na vijana wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Kaduma, UCSAF ina jukumu la kisheria la kuhakikisha wananchi wanaongeza ujuzi na matumizi ya teknolojia za habari na mawasiliano, hivyo wataendelea kutumia wataalamu waliobobea kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika jamii.

Akihitimisha, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutoa fursa za kujiendeleza kitaaluma kwa watumishi wa umma, akisema uwekezaji huo unachangia kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi na kuimarisha maendeleo ya taifa.

Pia alitoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwekeza katika elimu ya teknolojia kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla, ili kujenga jamii yenye ujuzi wa kidijitali na kuongeza ushindani wa Tanzania katika uchumi wa kisasa.





 

0/Post a Comment/Comments