Na Carlos Claudio, Dodoma.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma limezitaka jamii kutumia nishati safi ya kupikia kwa umeme ili kulinda afya, kuhifadhi mazingira na kupunguza gharama za matumizi ya nishati majumbani.
Hayo yamesemwa na Afisa Masoko Kwandamizi wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Doris Mfinanga, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Chamwino Arts Centre (CAC) kuelekea ufunguzi wa Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo unaotarajiwa kufanyika Julai 25, 2026, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule.
Mfinanga amesema TANESCO itakuwepo katika tamasha hilo kuanzia siku ya kwanza hadi mwisho kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme kupitia maonesho ya vitendo katika banda lao.
Amesema wananchi watapata fursa ya kujionea jinsi majiko ya kisasa ya umeme yanavyofanya kazi, huku yakitumia umeme mdogo kwa gharama nafuu, bila kutoa moshi na hivyo kulinda afya ya mpishi pamoja na mazingira.
"Majiko haya yana uwezo wa kupika vyakula vya aina zote za Kitanzania ikiwemo maharage, wali na makande kwa kutumia umeme mdogo sana, hata chini ya unit moja ambayo ni takribani shilingi 360. Hivyo hata chakula kinachochukua muda mrefu kama maharage kinaweza kupikwa kwa gharama ndogo," amesema Mfinanga.
Ameongeza kuwa TANESCO imechagua kushiriki tamasha hilo kutokana na kukutanisha maelfu ya wananchi na vikundi mbalimbali, hali itakayowezesha elimu ya matumizi ya nishati safi kuwafikia watu wengi zaidi.
"Tunaamini tamasha hili litakuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi zaidi ya 10,000 na kuwaelimisha kuhusu faida za kupikia kwa umeme, huku tukimuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini," amesema.
Aidha, amewakaribisha wananchi kutembelea banda la TANESCO ili kupata elimu pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.
Kwa upande wake, Afisa Msaidizi wa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Regina Mkalawa, amesema ushiriki wa shirika hilo katika Tamasha la Cigogo unalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu teknolojia za kisasa za kupikia kwa umeme.
Amesema TANESCO imejiridhisha na ubora wa majiko ya kisasa ya Pressure Cooker na Induction Cooker baada ya kuyafanyia tathmini ya kitaalamu na kubaini kuwa yanatumia umeme mdogo huku yakipika kwa haraka na ufanisi.
Mkalawa amesema hata wananchi wanaotumia umeme wa kiwango cha chini, hususan walio kwenye Tarifa 0wanaotumia chini ya unit 75 kwa mwezi, wanaweza kutumia majiko hayo kwa gharama nafuu.
Ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanapunguza muda wa kupika, huondoa usumbufu wa kutumia mkaa au kuni, hulinda afya kwa kuzuia moshi ndani ya nyumba na huchangia uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti.
Amesisitiza kuwa Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo limekuwa fursa muhimu kwa TANESCO kuendelea kuwafikia wananchi wengi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kama sehemu ya safari ya Tanzania kuelekea matumizi ya nishati endelevu.


Post a Comment