NA Ester Maile Dar es Salaam
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeibuka mshindi wa nafasi ya pili na kutunukiwa tuzo katika kipengele cha Banda Bora upande wa Sekta ya Miliki na Real Estate wakati wa sherehe za ufungaji wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya (Sabasaba) jijini Dar es Salaam yaliyofikia kilele chake leo Julai 13, 2026.
Tuzo hiyo imepokelewa kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud W. Kondoro, na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Amina Lumuli, ambaye amesema ushindi huo unatokana na ubunifu mkubwa uliooneshwa katika maandalizi ya banda la taasisi hiyo pamoja na namna lilivyofanikiwa kuwasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wananchi na wadau wa maendeleo.
Akizungumza na waandishi Wa habari Lumuli ameongeza kuwa TBA imeweka mkazo katika kuonesha fursa za uwekezaji kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), sambamba na kuelimisha wananchi kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa na wakala huo katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa miongoni mwa miradi iliyovutia wageni wengi waliotembelea banda la TBA ni pamoja na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, miradi ya majengo ya serikali pamoja na ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya michezo ikiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambayo imeendelea kuonesha uwezo wa kitaalamu wa taasisi hiyo katika sekta ya ujenzi na usimamizi wa majengo.
Lumuli amesema tuzo hiyo ni ishara ya kuendelea kuaminiwa kwa TBA na wananchi pamoja na wadau mbalimbali kutokana na huduma bora, ubunifu wa kihandisi na uwezo wa taasisi hiyo wa kutekeleza miradi yenye tija kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.
Sherehe za utoaji wa tuzo na ufungaji wa maonesho hayo zimeongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, huku TBA ikiendelea kutajwa miongoni mwa taasisi za serikali zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma.


Post a Comment