TEA YAIMARISHA MTAALA MPYA KUPITIA MAFUNZO YA AMALI

........

Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeeleza kuwa inaendelea kutafuta na kusimamia rasilimali fedha kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, hususan baada ya kuanza kutekelezwa kwa mtaala mpya ulioboreshwa.

Hayo yamesemwa na Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa TEA, Eliafile Solla, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 8, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Solla amesema TEA ni taasisi ya Serikali inayofanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ikiwa na jukumu la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa na kutafuta rasilimali za kusaidia kuboresha sekta ya elimu nchini.

Amesema baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mtaala mpya ulioboreshwa, mamlaka hiyo imejielekeza katika kutafuta fedha na rasilimali nyingine muhimu za kusaidia ufundishaji na ujifunzaji wa mtaala huo, ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya mafunzo ya amali.

“Katika Maonesho haya ya 50 ya Kimataifa ya Biashara, TEA tunashiriki kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi, kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yetu na kuonesha namna ambavyo tumeshiriki katika utekelezaji wa mtaala mpya, ujasiriamali na ukuzaji wa ujuzi,” amesema Solla.

Amesema banda la TEA limewakutanisha wananchi na wanufaika wa programu mbalimbali zinazosimamiwa na mamlaka hiyo, wakiwemo wanafunzi na walimu kutoka shule za sekondari jijini Dar es Salaam wanaonufaika na vifaa vya mafunzo ya amali ya ushoni.

Kwa mujibu wa Solla, wanafunzi hao wanatumia banda hilo kuonesha kwa vitendo namna wanavyotumia ujuzi wa kushona walioupata shuleni, baada ya shule yao kupatiwa vifaa vya kisasa vya mafunzo ya ushoni.

Pia, amesema katika banda hilo wapo wanufaika wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), unaosimamiwa na kuratibiwa na TEA, ambao wanatoa ushuhuda wa namna mafunzo ya ujuzi yalivyowasaidia kujiajiri, kuongeza uzalishaji na kutimiza ndoto zao.

Miongoni mwa wanufaika hao ni mjasiriamali Easther Shebe, ambaye amesema mafunzo aliyopata kwa gharama nafuu kupitia Taasisi ya Uendelezaji wa Viwanda Vidogo (SIDO) yamebadili maisha yake na kukuza biashara yake ya uzalishaji wa uyoga.

Shebe amesema kabla ya kupata mafunzo hayo hakuwa na uzalishaji mkubwa wala bidhaa za kutosha, lakini sasa anaweza kuzalisha aina mbalimbali za uyoga, ikiwemo uyoga mwekundu, oyster nyeupe, oyster ya njano na oyster ya pink.

Ameishukuru TEA kwa kusimamia mfuko huo na kuwezesha wananchi kupata mafunzo ya kuendeleza ujuzi, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiwezesha sekta ya elimu na ujuzi nchini.

Kwa upande wao, wanafunzi wa mkondo wa amali ya ushoni kutoka Shule ya Sekondari Dar es Salaam wamesema mafunzo hayo yamewapa fursa ya kupata ujuzi wa kujiajiri sambamba na kuendelea na masomo ya darasani.

Mwanafunzi Emiliano Shauri amesema masomo ya amali ya ushoni yamemsaidia kujifunza kushona sare za shule, mashati, suruali, gauni na sketi, huku akieleza kuwa mashine za kisasa walizopewa zimepunguza gharama na kurahisisha mafunzo ya vitendo.

Naye Maria Richard amesema kuanzishwa kwa mkondo wa amali kunawawezesha wanafunzi kujiajiri baada ya kumaliza masomo na hivyo kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.

Amesema vifaa vya kushonea vya kielektroniki vilivyotolewa na TEA vimewarahisishia mafunzo, tofauti na awali ambapo walilazimika kwenda katika vyuo vya VETA kupata mafunzo ya vitendo.

Mwalimu wa mkondo wa amali ya ushoni katika shule hiyo, Rosana Magubika, ameishukuru TEA kwa kutoa mashine na vifaa vya mafunzo, akiiomba mamlaka hiyo kuendelea kuzifikia shule nyingine pamoja na kuongeza mashine za kufumia sweta.

TEA imewataka wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu Mfuko wa Elimu wa Taifa, Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi na fursa mbalimbali za ushirikiano katika kuimarisha elimu, ujuzi na ujasiriamali nchini.

 








 

0/Post a Comment/Comments